Umaskini umekithiri miongoni mwa makabila na makundi fulani duniani

7 Oktoba 2021

Watu bilioni 1.3 katika nchi 109 duniani ni maskini wa kila hali na kiwango cha umaskini huo kinatofautiana kikabila, kwa kundi au rangi, hiyo ni kwa mujibu wa uchambuzi mpya kuhusu kiwango cha umaskini wa kila hali duniani ikiwemo kiafya, kielimu na kiwango cha maisha, uliotolewa leo na Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. 

Ripoti hiyo inatokana na utafiti wa pamoja wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP na taasisi ya Oxford ya kupima umaskini na maendeleo katika nchi 109 ambapo nchi 41 zimewasilisha taarifa za kina kuhusu makabila ya watu, rangi zao na makundi waliyotengewa katika jamii.  

Tofauti ya umaskini inaendana na kabila, rangi au kundi  

Kilichobainika ni kwamba tofauti ya umaskini miongoni mwa makabila ni kubwa katika nchi nyingi duniani na katika makabila 9 zaidi ya asilimia 90 ya watu wake wamenasa kwenye lindi la umaskini   

“Ripoti imegundua kuwa “katika baadhi ya maeneo, tofauti za kiwango cha umaskini wa kila hali ni kikubwa kwa baadhi ya makabila na rangi fulani ikilinganishwa na maeneo mengine ya kijiografia. Halikadhalika hata ndani ya nchi kuna tofauti kubwa miongoni mwa makabila,”   

Mathalani katika makabila nchini Gabon na Nigeria tofauti za kiwango cha watu ambao ni maskini kwa kila hali ni kikubwa na kinafikia asilimia 70. Huko Amerika ya Kusini, jamii za watu wa asili ndio mafukara na hohehahe ,ripoti ikitolea mfano Bolivia ambako jamii za watu wa asili ni asilimia 44 na miongoni mwao hao, asilimia 75 ni maskini wa kila hali na wanatoka makabila na makundi duni.  

Nchini India nako takwimu zinatia hofu ambako watu 5 kati ya 6 ambao ni maskini kwa kila hali wanatoka katika makabila duni.  

Nchini india watu watano kati ya sita walio maskini wa kila hali wanatoka katika makabila au makundi ya jamii duni.
UNDP India/Dhiraj Singh
Nchini india watu watano kati ya sita walio maskini wa kila hali wanatoka katika makabila au makundi ya jamii duni.

Ambako mwanamke hajaenda shule idadi ya maskini ni kubwa  

Ikiangazia umaskini na maisha duni kijinsia, ripoti inasema duniani kote theluthi mbili ya watu maskini wa kila hali sawa na watu milioni 836, wanaishi katika kaya au familia ambako hakuna mwanamke au mtoto wa kike aliyehitimu angalau miaka sita ya elimu ya msingi.  

Halikadhalika watu milioni 215 walio mafukara wanaishi kwenye kaya au familia ambako angalau mwanaume au mvulana mmoja amehitimu miaka sita ya elimu ya msingi au zaidi huku hakuna mwanamke au msichana hata mmoja aliyekwenda shule.  

Ikimulika ukatili wa kijinsia, ripoti inasema mwanamke au msichana aliye katika lindi la umaskini yuko hatarini zaidi kupata mwandani mnyanyasaji.  

Kipimo cha umaskini wa kila hali mwaka 2021
Multidimensional Poverty Index 2021
Kipimo cha umaskini wa kila hali mwaka 2021

Nusu ya maskini wa kila hali ni watoto  

Miongoni mwa watu wote bilioni 1.3 ambao ni maskini wa kila hali, takribani nusu yao sawa na milioni 644 ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 18. Halikadhalika zaidi ya asilimia 85 ya watu hao maskini wako katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na  zile za Asia Kusini. 

Nchi 5 ambako maskini wengi wa kila hali wanaishi ni India, Nigeria, Pakistan, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Ripoti inafafanua kuwa zaidi ya asilimia 67 ya maskini wa kila hali wanatoka nchi za kipato cha kati.  

Maisha ya kila siku ya watu maskini wa kila hali yako vipi  

Ripoti inasema watu hao wanatumia nishati isiyo rafiki kwa afya zao na mazingira yao, huduma za kujisafi na usafi hazitoshi na makazi yao ni duni.  

“Watu milioni 788 wa kundi hilo wanaishi na angalau mwanafamilia mmoja mwenye lishe duni, milioni 568 wanakosa maji safi na salama katika eneo lao mwendo wa nusu saa kwenda na kurudi kutoka makazi yao.”  

Kiongozi Mkuu wa UNDP Achim Steiner akizungumzia ripoti hiyo amesema, janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limemomonyoa maendeleo duniani kote, “nab ado tunaendelea kuhaha kutambua athari zake. Kipimo cha sasa cha umaskini wa kila hali kinatukumbusha umuhimu wa kuwa na taswira halisi ya jinsi watu wanaathiriwa na umaskini, ni watu wa aina gani, wanaishi wapi  iwapo tunataka kujenga na kuibuka kwa ubora zaidi baada ya COVID-19 na tusimwache nyuma mtu yeyote.”  

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter