Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji wa haki za binadamu DRC umepungua mwaka 2020/2021

Watoto waliofurushwa Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
© UNICEF/Olivia Acland
Watoto waliofurushwa Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Ukiukwaji wa haki za binadamu DRC umepungua mwaka 2020/2021

Haki za binadamu

Hali ya haki za binadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC bado inatia wasiwasi ingawa idadi ya matukio ya ukiukwaji huo yamepungua, imesema ripoti ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ripoti aliyowasilisha leo huko Geneva, Uswisi kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu, HRC.
 

Ikiangazia kipindi cha kuanzia tarehe 1 Juni mwaka 2020 hadi tarehe 31 mwezi Mei mwaka 2021, ripoti hiyo imeandaliwa na ofisi ya pamoja ya haki za binadamu na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  na inaonesha kuwa, “ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili vimepungua kwa asilimia 3 ikilinganishwa na kipindi kilichotanguliwa cha mwaka 2019/2020 ingawa kiwango cha ukiukwaji wa haki na madhara ya vitendo hivyo bado ni makubwa kwa jamii.”

Ripoti imesema wakati wa kipindi hicho cha Juni 2020 hadi Mei 2021, takribani watu 718  ikiwa ni wanawake 492, watoto 218 na wanaume 8 ndio walikuwa manusura wa ukatili wa kingono nchini DRC. Takwimu  hizi ni pungufu kubwa ikilinganishwa na mwaka uliotangulia ambapo kulikuwa na matukio 1,376 huku jimbo la Kivu Kaskazini ndio likiwa na matukio mengi zaidi ya visa vya ukatili wa kingono kwenye maeneo ya Masisi, Rutshuru na Nyiragongo.”

Asilimia 46 ya matukio hayo ya ukiukwaji wa haki yametekelezwa na maafisa wa serikali, hususan wanajeshi wa jeshi la serikali, FARDC pamoja na polisi.

Mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami nayo yamepungua huko jimboni Kivu Kaskazini, Ituri na Kivu Kusini ingawa ripoti inasema kuwa matukio hayo yamesambaa katika maeneo mapya ya majimbo hayo kutokana na kauli za chuki na vitendo vya kuchochea ghasia.

Wanawake wakiwa wamekusanyika katika kituo cha kugawa chakula cha Nyanzale Kivu Kaskazini DRC. Kituo hicho kinawalenga kwa msaada familia zisizojiweza na zilizo hatarini
OCHA/Ivo Brandau
Wanawake wakiwa wamekusanyika katika kituo cha kugawa chakula cha Nyanzale Kivu Kaskazini DRC. Kituo hicho kinawalenga kwa msaada familia zisizojiweza na zilizo hatarini

Ripoti inaweka bayana kuwa ukiukwaji wa haki ya kidemokrasia umepungua. “Kufunguliwa kwa milango ya demokrasia kulikoanza mapema mwaka 2019 kumeendelea hadi kipindi cha sasa na kuwezesha kupungua kwa ukiukwaj iwa haki za kiraia na kisiasa. Ingawa mashambulizi na vitisho dhidi ya waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati vimeendelea sambamba na ubinyaji wa haki ya kuandamana kwa amani kwa kisingizio cha udhibiti wa kusambaa kwa virusi vya Corona au COVID-19 na hali ya hatari iliyotangwa na Rais Felix Tshisekedi kuanzia tarehe Machi mwaka jana.” imesema ripoti hiyo.

Mapendekezo ya Kamishna Mkuu kwa serikali ya DRC

Katika ripoti hiyo ya kurasa 14 Kamishna Mkuu Bachelet ametoa mapendekezo 16 ikiwemo serikali iendelee kufungua milango ya demokrasia na kuhakikisha inalinda uhuru na haki za msingi za wapinzani wa kisiasa, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu na makundi ya asasi za kiraia.

Serikali itunge sheria ya kuanzisha hatua za kulinda haki ya kuandamana kwa amani kwa mujibu wa Katiba ya nchi na sheria za kimataifa. Halikadhalika matumizi ya nguvu za kijeshi yazingatie kanuni za kimataifa, ichunguze wanajeshi wanaodaiwa kuhusika na ukatili wa kingono ili sheria ichukue mkondo wake, na pia ichukue hatua zote zinazohitajika kuzuia ukatili wa kingono na pindi unapotokea wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa imesema kwa upande wake itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya DRC za kutekeleza ahadi zake za kuzingatia haki za binadamu hususan kwenye maeneo ya marekebisho ya sheria na kujengea uwezo watumishi wa serikali na wale wa mashirika ya kiraia.