Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za maji zinaongezeka duniani:WMO Ripoti

Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa linasema mtu mmoja kati ya watatu duniani kote amekumbwa na shida ya uhaba wa maji
© UNICEF/Saleh Hayyan
Shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa linasema mtu mmoja kati ya watatu duniani kote amekumbwa na shida ya uhaba wa maji

Changamoto za maji zinaongezeka duniani:WMO Ripoti

Tabianchi na mazingira

Usimamizi bora wa maji ni muhimu, pamoja na ufuatiliaji na tahadhari ya mapema, vingesaidia kupunguza shida zinazosababishwa na wingi auuhaba wa bidhaa hiyo adimu, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO.

Ripoti inasema mafuriko, ukame na majanga mengine yanayohusiana na maji yanaongezeka kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi na, ukizingatia ongezeko la idadi ya watu duniani na kupungua kwa upatikanaji wa rasilimali hiyo katika maeneo mengi, na idadi ya watu wanaoathirika na matukio haya itaongezeka, limeonya shirika hilo la WMO.

Katika utafiti huo mpya, WMO inaonya juu ya usimamizi uliogawanyika na duni wa maji na inaangazia rasilimali za kutosha kukabiliana na hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi ambayo dunia inapitia hivi sasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna haja ya dharura ya kuboresha ushirika wa usimamizi wa maji, kupitisha sera zilizojumuisha masuala ya maji na mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza uwekezaji katika mali hii ya thamani ambayo ni muhimu katika malengo yote ya kimataifa ya maendeleo endelevu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hatari za majanga yanayohusiana na maji..

Mfumo wa mvua hubadilika

Ripoti hiyo inaelezea kuwa mabadiliko ya  mvua kimataifa na kikanda  kwa sababu ya ongezeko la joto duniani yanabadilisha mwelekeo wa mvua na msimu wa kilimo, na kuathiri uhakika wa chakula na ustawi wa binadamu.

2021 State of Climate Services: Water - English

Katibu Mkuu wa WMO amekumbusha kuwa matukio mabaya yanayohusiana na maji yalitamalaki mwaka jana.

"Mvua kubwa zilisababisha mafuriko makubwa nchini Japani, Uchina, Indonesia, Nepal, Pakistan na India. Mamilioni ya watu walihama makazi yao na mamia walikufa. Lakini sio tu katika nchi zinzoendelea ambako mafuriko yamesababisha usumbufu mkubwa. Mafuriko mabaya huko Ulaya pia yalisababisha mamia ya vifo na uharibifu mkubwa, "amesema Petteri Taalas.

Ameongeza kuwa ukosefu wa maji unabaki kuwa sababu kuu ya hofu kwa mataifa mengi, haswa barani Afrika, ambapo zaidi ya watu bilioni mbili wanaishi katika nchi zilizo na shida ya maji na kukosa huduma ya maji salama na usafi wa mazingira.

Lazima tuamke

"Tunahitaji kuamka kutokana na changamoto ya maji inayokuja," amesisitiza Taalas.

WMO inakadiria kuwa watu bilioni 3.6 waliishi bila upatikanaji wa kutosha wa maji kwa angalau mwezi mmoja kwa mwaka mnamo mwaka 2018 na inatabiri kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi hiyo itazidi watu bilioni 5.

Jumla ya maji yote ya juu ya uso wa dunia na katika chini ya ardhi, ambayo ni pamoja na barafu, yamepungua kwa sentimita moja kila mwaka katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita na hali inazidi kuwa mbaya kwani asilimia 0.5% ya maji hayo ndiyo yanaweza kutumika kama maji safi.

Kwa kuongezea,ripoti inasema tangu mwaka 2000, majanga yanayohusiana na mafuriko yameongezeka kwa asilimia 134% ikilinganishwa na miongo miwili iliyopita.

Vifo vingi vimetokea napia  hasara za kiuchumi kutokana na mafuriko yalitokea Asia, ambapo mifumo ya tahadhari ya mapema inahitaji kuimarishwa.

Kwa upande mwingine, idadi na muda wa ukame uliongezeka kwa asilimia 29% katika kipindi hicho hicho.

Kwa mujibu wa ripotoi idadi kubwa ya vifo vya ukame viko barani Afrika, ikionyesha kwamba bara hilo pia linahitaji mifumo imara ya tahadhari.

Ripoti hiyo inasema kuwa kufanikisha ustawi wa muda mrefu wa kijamii, uchumi na mazingirakunahitajika usimamizi jumuishi wa rasilimali za maji.

Lakini imeongeza kuwa , nchi 107 haziko kwenye njia sahihi kufikia lengo la kusimamia rasilimali zao za maji endelevu ifikapo 2030.

Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo
© UNICEF/Scott Moncrieff
Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo

Mapendekezo

WMO imetoa mapendekezo kadhaa kwa watunga sera ili kuboresha ufanisi wa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya maji ulimwenguni kote:

• Imetaka dunia kuwekeza katika usimamizi wa rasilimali za maji kama suluhisho la kudhibiti shida za maji, haswa katika nchi zinazoendelea za visiwa vidogo na nchi zilizoendelea.

• Imetaka kuwekeza katika mifumo ya utoaji wa tahadhari za mapema kwa suala la  ukame na mafuriko katika nchi zilizoendelea zilizo hatarini zaidi, pamoja na tarifa za ukame barani Afrika na maonyo ya mapema ya mafuriko huko Asia.