COVID-19 inaacha kovu la kudumu katika afya ya akili ya watoto na vijana

5 Oktoba 2021

Watoto na vijana watasalia na madhara ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa afya zao za akili na kimwili kwa miaka mingi ijayo, imesema ripoti mpya ya hali ya watoto duniani  SOWC ilyotolewa leo jijini New York, Marekani na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni, UNICEF. 

Ripoti hiyo ikijikita kwa kina katika afya ya akili kwa watoto, vijana na walezi katika karne ya 21 imesema hata kabla ya janga la Corona, watoto na vijana walibeba mzigo wa matatizo ya afya ya akili bila kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha kutatua tatizo hilo. 

Makadirio mapya yanaonesha kuwa zaidi ya barubaru 1 kati ya 7 wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 17 anaishi na ugonjwa wa afya ya akili. Takribani barubaru 46,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua, moja ya sababu kuu 5 za vifo miongoni mwa kundi hilo. 

Kuvurugwa kwa ratiba za maisha, elimu na michezo sambamba na hofu ya kipato cha familia na afya, kumeacha watoto na vijana kuogofya, kuchukia na wasiwasi kuhusu maisha yao ya baadaye - Ripoti

Hata hivyo bado kuna pengo kati ya afya ya akili na uwekezaji wa fedha katika sekta ya afya ya akili ambapo ripoti imebaini kuwa asilimia 2 ya bajeti ya serikali ndio inaelekezwa kwenye afya ya akili duniani kote. 

“Miezi 18 ya Corona ni muda mrefu kwetu sote, hasa kwa watoto. vizuizi vya kutembea vilivyowekwa katika nchi il ikudhibiti Corona, vimefanya watoto wawe mbali na familia zao, marafiki, madarasa yao bila kusahau michezo, mambo ambayo ni ya msingi katika ukuaji wa mtoto,” amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF

Ameongeza kuwa madhara yake ni makubwa na kinachoonekana sasa ni taswira ndogo ya hali halisi “Kwa kuwa hata kabla ya Corona, watoto walikuwa wametishwa mzigo wa matatizo ya afya ya akili ambayo hayakushughulikiwa. Fedha zinazotengwa ni kidogo na pia uhusiano kati ya afya ya akili na ustawi wa baadaye wa mtoto nao hautiliwi maanani.” 

Sheila Achieng, akiwa kwenye masomo yake nyumbani huko Kibera kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
© UNICEF/Brian Otieno
Sheila Achieng, akiwa kwenye masomo yake nyumbani huko Kibera kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Afya ya watoto wakati wa COVID-19 

Utafiti wa UNICEF na Gallup katika nchi 21 umebaini kuwa kijana kati ya 1 hadi 5 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 mara nyingi walikuwa na msongo wa mawazo au hawakuwa na hamu ya kufanya kitu chochote. 

Ugonjwa wa Corona ukiingia mwaka wa tatu, takwimu zinaonesha kuwa mtoto 1 kati ya 7 duniani kote ameathirika moja kwa moja na vizuizi vya kutembea, huku zaidi ya watoto milioni 1.7 wameathirika kwa kukosa elimu. Kuvurugwa kwa ratiba za maisha, elimu na michezo sambamba na hofu ya kipato cha familia na afya, kumeacha watoto na vijana kuogofya, kuchukia na wasiwasi kuhusu maisha yao ya baadaye. 

Ripoti imenukuu utafiti uliofanyika China ukionesha kuwa theluthi moja ya walioshiriki kwenye utafiti waliripoti kuwa na uoga au wasiwasi. 

Na huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mvulana mmoja amenukuliwa akisema kuwa akiwaza juu ya idadi ya watu waliokufa kutokana na COVID-19 anaumia mno, na apatapo taarifa kuwa idadi ya wagonjwa inaongezeka, hilo sasa linampatia msongo wa mawazo.

Gharama kwa jamii 

Magonjwa ya akili ikiwemo kiwewe, usonji, ulaji kupindukia, msongo wa mawazo yanaathiri vijana na watoto kiafya, kielimu, ustawi wa baadaye na uwezo wa kujipatia kipato. 

Ripoti inasema wakati madhara ya kiafya hayawezi kupimika, uchambuzi mpya umegundua kuwa kushindwa kuchangia kiuchumi kutokana na tatizo la afya ya akili linalosababisha vifo au ulemavu miongoni mwa vijana kunagharimu uchumi kwa dola takribani bilioni 390 kila mwaka. 

Ninapofikiria juu ya kila mtu aliyekufa kwa sababu ya Corona, inaniumiza sana, na nipatapo taarifa kuwa idadi ya wagonjwa inaongezeka, hiyo inanipa msongo wa mawazo- Mvulana DRC

Visababishi vya afya ya akili bora au dhaifu 

Ripoti inasema kuwa jeni za mwili, uzoefu wa maisha na mazingira kuanzia utotoni ikiwemo malezi ya wazazi, shule, uhusiano, ghasia, ukatili, ubaguzi, umaskini, majanga ya kibinadamu  na dharura za kiafya kama vile COVID-19 vinachangia katika afya ya akili ya akili ya mtoto katika kipindi chote cha maisha yake. 

Ni kwa mantiki hiyo ripoti inapendekeza mambo muhimu matatu ya kufanywa na serikali na sekta binafsi ikiwemo, mosi; kuwekeza katika afya ya akili kwa vijana na watoto, kujumuisha hatua za kuchukua katika sekta zote iwe shuleni, nyumbani au hospitalini ili kusaidia afya njema ya akili na tatu kuvunja ukimwa unaozingira magonjwa ya akili kwa kuondoa unyanyapaa dhidi ya wagonjwa na kuzingatia uzoefu wa watoto na vijana katika suala hilo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF anatamatisha akisema ,”afya ya akili ni sehemu ya afya ya mwili, hatuwezi kuendelea kuona vinatengeshwa. Kwa muda mrefu katika nchi tajiri na maskini tumeshuhudia uelewa mdogo au uwekezaji mdogo katika suala hili ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto. Hii lazima ibadilike.” 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter