Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madeni kwa nchi maskini ni ‘kisu’ katikati ya moyo wa kujikwamua kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia ufunguzi wa mkutano wa 15 wa UNCTAD huko Bridgetown, Barbados
UN Barbados and the Eastern Caribbean/Bajanpro
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia ufunguzi wa mkutano wa 15 wa UNCTAD huko Bridgetown, Barbados

Madeni kwa nchi maskini ni ‘kisu’ katikati ya moyo wa kujikwamua kiuchumi

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amefungua mkutano wa 15 wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara, UNCTAD15 huko nchini Barbados kwa kutangaza mambo makuu manne ya kusaidia kukabiliana na janga la madeni linalogubika nchi maskini wakati huu ambapo zinahaha kujikwamua kutoka katika janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Guterres ametangaza mambo hayo manne kwa kutambua kuwa “machungu yanayokumba nchi maskini kutokana na madeni yaliyozigubika ni sawa na kisu kinachochoma kwenye moyo wa dunia wa kujikwamua. Nchi haziwezi kujijenga upya vyema iwapo zitarudishwa nyuma na madeni.”

Katibu Mkuu amesema anaunga mkono tangazo la hivi karibuni la shirika la fedha duniani, IMF la kutenga dola bilioni 650 kwenye mpango wa haki mahsusi za ukopaji, SDR, “lakini msaada huu kwa kiasi kikubwa unakwenda kwa nchi ambazo hazihitaji fedha hizo kwa sababu mgao wake unafanyika kwa misingi ya vigezo vya uwezo.”

Mambo 4 ya kuondokana na janga la madeni

Kwa mantiki hiyo jambo la kwanza “leo natoa wito kwamba fedha za SDR ambazo hazijatumika zielekezwe kwenye nchi zilizo hatarini zaidi na zinazohitaji fedha hizo zikiwemo zile za kipato cha kati. Pili tunafahamu kuwa nchi zinatwamishwa na gharama za ulipaji madeni, kwa hiyo tunahitaji kuongezwa muda zaidi wa mpango wa kundi la nchi 20 au G20 wa kusitisha ulipaji madeni hadi mwaka kesho. Mpango wao unasaidia kupunguza janga la madeni.”

Msaada wa mpango wa SDR unanufaisha nchi zisizohitaji msaada huo. Tafadhali elekezeni fedha hizo kwa nchi ambazo zina uhitaji zaidi zikiwemo zile za kipato cha kati- António Guterres, Katibu Mkuu UN.

Bwana Guterres amesema usitishaji kwa muda ulipaji wa madeni unapaswa kuendelea hadi mwakani na pia mpango huo uhusishe nchi zote zinazohitaji ikiwemo zile za kipato cha kati.

Jambo la tatu amesema “tunatambua kusitisha ulipaji madeni si jawabu linalotosheleza kwa nchi zote. Nchi zitahitaji unafuu wa madeni unaohusisha wadeni wa umma na wale wa kibinafsi.”

Ili kufanikisha hilo Katibu Mkuu amerejelea wito wake wa kuangaliwa upya kwa mfumo wa kimataifa wa ukopeshaji ikiwemo kupunguza madeni hasa kwa nchi za kipato cha kati ili ziweze kuondoka katika mzunguko mbaya wa madeni.

Jambo la nne ni ufadhili kutoka sekta binafsi akisema “si jambo la haki kabisa kuona nchi tajiri zinaweza kukopa kwa unafuu na kujikwamua kwa urahisi ilhali nchi za kipato cha chini na kati zinahaha kuimarisha uchumi wao. Tunahitaji kuleta pamoja sekta ya umma na sekta binafsi ili kuendeleza mbinu bunifu za ufadhili za kuchochea kurejea kwa vitegauchumi vya sekta binafsi kama ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19, hali ambayo itatochea kujikwamua kiuchumi.”

Guterres amesema mambo hayo manne yatasaidia kuhakikisha hakuna serikali inalazimika kuchagua kati ya kulipa deni na kuhudumia wananchi wake.

Mkutano mkuu wa UNCTAD hufanyika kila baada ya miaka 4 na mara ya mwisho  UNCTAD14 ulifanyika jijini Nairobi nchini Kenya mwaka 2016.