Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yachukua Urais wa Baraza, Balozi Omamo atoa msimamo kuhusu wakimbizi

Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.
WFP
Wakimbizi wapanga foleni kupokea mgao wa chakula katika kambi ya Kakuma Kaskazini mwa Kenya.

Kenya yachukua Urais wa Baraza, Balozi Omamo atoa msimamo kuhusu wakimbizi

Masuala ya UM

Kenya ambayo imechukua urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Oktoba imesema itakuwa na mikutano minne ya ngazi ya juu ambapo miwili itahutubiwa na Rais Uhuru Kenyatta ilhali mingine miwili itakuwa ni ngazi ya mawaziri na kuhutubiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo la Afrika Mashariki Balozi Raychelle Omamo.
 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja huo Balozi Martin Kimani amesema Rais Uhuru ataongoza mijadala ya ngazi ya juu kuhusu ujenzi wa ujenzi na uendelezaji wa amani pamoja na hali katika ukanda wa maziwa makuu.

Kwa upande wake Balozi Omamo ataongoza mijadala kuhusu Wanawake, amani na usalama pamoja na Mashariki ya Kati. 

Msimamo wetu ni huu kuhusu wakimbizi

Alipoulizwa kuhusu suala la wakimbizi wa Somalia walioko nchini Kenya na hatma yao kwenye kambi nchini humo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya ambaye pia ameshiriki mkutano huo amesema, Balozi Raychelle Omamo “kambi za wakimbizi hazipaswi kuwa ndio suala la kudumu. Kwa mtazamo wetu wa haki za binadamu, ni ukiukwaji mkubwa wa haki kuwaweka watu katika mazingira tata kwenye kambi maisha yao yote.”

Tweet URL

Hivyo akasema “hisia zetu ni kwa vipi tutakuwa na mtazamo mpana kuhusu kambi za wakimbizi, tufikirie kuhusu suluhisho la tatu na pia kufikiria njia za kujumuisha wakimbizi kama inawezekana, na vile vile kufikiria kurejea kwa wakimbizi kwa hiari nyumbani kwao bila kukiuka misingi ya urejeshaji, na kuhakikisha kuwa wakimbizi wanarejea sehemu  ambako kuna amani, sehemu ambazo zina amani. Huu ni mjadala ambao tunapaswa kuwa nao kama jamii ya kimataifa."

Balozi Omamo amesema kuna binadamu wengi ambao wanaishi kwenye kambi za wakimbizi maisha yao yote bila matumaini yoyote na katika hali ya kukata tamaa. “Kwa hiyo huu ndio msimamo wetu  ambao tunataka kuelezea watu tujadiliane ili tuwe na mtazamo mpya kwa watu walio hatarini na kwa watu ambao wanakimbia makwao.”

Mwezi Aprili mwaka huu wa 2021, Kenya ilitangaza kuwa itafunga kambi za Daadab na Kakuma ifikapo mwezi Juni mwaka 2022, hatua ambayo ilifuatiwa na mazungumzo kati ya Kenya na Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Fillipo Grandi ambapo pande zote mbili zilikubaliana kuwa kambi si suluhisho la kudumu na zinafanyia kazi mpango wa kusaidia wakimbizi kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa wakimbizi, Global Compact on Refugees.

Kenya imeanza uanachama wake kwenye Baraza la Usalama tarehe Mosi mwezi Januari mwaka huu, uanachama utakaodumu kwa miaka miwili. Hata hivyo urais wa Baraza ni kwa mwezi mmoja miongoni mwa nchi 15 wanachama wa Baraza hilo la Usalama.

Ziara mashinani

Kwa mara ya kwanza tangu kuibuka kwa janga la Corona au COVID-19 mwaka jana na kusababisha Baraza la Usalama kusitisha ziara zake mashinani, mwezi huu wajumbe wa Baraza watakuwa na ziara kwenye ukanda wa Sahel ambapo kwa mujibu wa Balozi Kimani wajumbe watatembelea Mali na Niger.

Ethiopia nayo itakuwemo

Kwa mujibu wa Balozi Kimani katika ajenda ya mengineyo, suala la Ethiopia hususan mgogoro jimboni Tigary pia litajadiliwa.