Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 139 zahitajika kunusuru jamii za maeneo kame Kenya

Mtu akisaka maji kwenye moja ya maeneo kame Mashariki mwa Kenya
World Bank/Flore de Preneuf
Mtu akisaka maji kwenye moja ya maeneo kame Mashariki mwa Kenya

Dola milioni 139 zahitajika kunusuru jamii za maeneo kame Kenya

Msaada wa Kibinadamu

Ombi la dharura la dola milioni139.5 limezinduliwa hii leo na Umoja wa Mataifa ili kusaidia wakazi wa maeneo kame zaidi nchini Kenya.
 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imetangaza ombi hilo likilenga kusaidia milioni 2.5 wanaoishi kwenye maeneo kame ya Kenya, ASAL.

Watu hao, kwa mujibu wa OCHA wamekuwa wanakumbwa na ukosefu wa uhakika wa chakula kutokana na ukosefu wa mvua kwa miaka miwili mfululizo.

“Hadi mwezi ujao wa Novemba, idadi hiyo inaweza kuongezeka mara tatu tangu kiwango kama hicho mwaka jana, “ imeonya OCHA.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Stephen Jackson akizindua ombi hilo leo jijini Nairobi, Kenya amesema, “watu katika maeneo hayo kame, au ASAL tayari wanakumbwa na hali mbaya ya kibinadamu.”

Bwana Jackson, akitolea mfano eneo la Wajir, kaskazini mwa Kenya ambako alitembelea, amesema, “wakazi wa eneo hilo hawajapata mvua kwa zaidi ya mwaka mzima. Viwango vya utapiamlo uliokithiri vinaongezeka kwa kazi kubwa na kutia hatarini afya ya watoto na akina mama wanaonyonyesha na wale wajawazito”

Maisha mashakani

Ameelezea jinsi mama mmoja katika kliniki ya El-Nur inayopatiwa msaada na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na la kuhudumia watoto, UNICEF alivyosimulia masaibu yake “siwezi kumpatia mwanangu mlo wa asubuhi na sijui ninaweza kumpatia mlo wa usiku.”

Mama huyo alisema kuwa mifugo yake imekufa kutokana na ukame na hali ya sasa imekuja ikifuatia ukame wa mwaka 2017, janga la ugonjwa wa Corona, COVID19 na baa la nzige la hivi karibuni.
“Nilikutana na wanawake, wanaume na watoto ambao wamenieleza jinsi maisha yao yanavyotwamishwa na ukame.”

Mratibu huyo mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya amesema ni vyema kuchukua hatua sasa kwa kushirikiana na jamii na mashirika ya kijamii ili kupunguza machungu kwa raia yaliyochochewa na mfululizo wa vipindi vya ukosefu wa mvua na kwamba  iwapo mvua za mwezi huu nao hazitanyesha Kenya inatarajiwa kuwa na janga kubwa.

Ombi la dharura kwa Kenya

Ni kwa mantiki hiyo wametoa ombi la dola milioni 139.5 ili kufikisha misaada kwa watu milioni 1.3 ambao maisha yao yameathiriwa zaidi na janga la sasa.

Takribani dola milioni 28.5 zimepokewa kutoka kwa wahisani, ikiwemo dola milioni 5 kutoka mfuko wa dharura wa misaada wa Umoja wa Mataifa, CERF.
Ombi hilo la fedha linajumuisha mashirika 45 yakiwemo ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia za kimataifa, za kitaifa  kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali.

Mahitaji yanaongezeka

Bwana Jackson ameweka bayana kuwa tayari serikali ya Kenya imechukua hatua. Dola milioni 17 zilishatengwa na serikali imetengaza nyongeza ya dola milioni 20.

Tangu mwezi Januari mwaka huu, Umoja wa Mataifa na wadau wake wamefikia watu 500,000 kwa kuwapatia misaada ya kuokoa maisha na kujipatia kipato lakini bado haitoshi, amesema Bwana Jackson.

Kwa mujibu wa mratibu huyo mkazi, Kenya inahitaji dola takribani milioni 60 kwa ajili ya chakula na uhakika wa ajira, dola milioni 40 kwa ajili ya lishe, dola milioni 20 kwa ajili ya maji na huduma za kujisafi, (WASH) na dola milioni 10 kwa uwekezaji katika sekta ya afya, dola milioni 7 kwa ajili ya elimu na sekta inazohusiana nazo.

“Tunalenga kufikisha msaada kamili kwa kaunti ambazo zitakumbwa na madhara zaidi katika miezi ijayo,” amesema Bwana Jackson.