Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Jamii ya wakulima huko katika bahari ya Pasifiki Archipelago, Vanuatu, wanakabiliana na hali ya hewa ya ukavu

Vijana endeleeni kupaza sauti kuokoa mazingira- Guterres

©UNICEF/Josh Estey
Jamii ya wakulima huko katika bahari ya Pasifiki Archipelago, Vanuatu, wanakabiliana na hali ya hewa ya ukavu

Vijana endeleeni kupaza sauti kuokoa mazingira- Guterres

Tabianchi na mazingira

Wakati janga la tabianchi tayari likiwa limeleta madhara kwa maisha na vipato va watu kote ulimwenguni, vijana watakuwa na nafasi muhimu zaidi katika kusongesha mbele hatua mujarabu, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa vijana wanaoshiriki mkutano tangulizi wa COP-26 huko mjini Milano nchini Italia. 

Mamia ya wajumbe vijana kutoka nchi mbalimbali duniani wanashiriki mkutano huo tangulizi wa mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi Novemba huko Glasgow Scotland. 

Tahadhari kwa ubinadamu 

“Vijana wamekuwa mstari wa mbele kuweka majawabu chanya, wakidai harakati za haki dhidi ya tabianchi na kuwajibisha viongozi wao. Tunahitaji vijana kila mahali wapaze sauti zao,” amesema Katibu Mkuu kupitia ujumbe wake aliotuma kwa njia ya video. 

Katibu Mkuu ameelezea dharura ya tabianchi kama hadhari kuu kwa binadamu ambapo walio hatarini zaidi tayari wamedhurika zaidi. 
“Dirisha la fursa ya kuzuia madhara mabaya zaidi ya janga la tabianchi linafunga haraka. Tunafahamu kile kinachopaswa kufanyika na tuna mbinu za kufanya,” amesema Bwana Guterres 

Picha ya maktaba iliyopigwa mwaka 2019 ikionesha vijana wakiwa wameandamana wakipaza sauti kuhusu mabadiliko ya tabianchi
ICAN/Lucero Oyarzun
Picha ya maktaba iliyopigwa mwaka 2019 ikionesha vijana wakiwa wameandamana wakipaza sauti kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Tekelezeni ahadi 

Katibu Mkuu amesihi viongozi vijana wa masuala ya tabianchi waendelee kupaza sauti ili kufikia makubaliano ya hatua za kuhimili majanga na kujenga mnepo ili kuhakikisha angalau asilimia 50 ya usaidizi wa shughuli za kulinda tabianchi unapatikana kwa lengo la kulinda maisha na mbinu za kujipatia kipato. 

Amefafanua sababu ya sauti za vijana kuhitajika hivi sasa ikiwemo nchi tajiri kutekeleza hatimaye ahadi zao za muongo mmoja za kuchangia dola milioni 100 kila mwaka katika ufadhili wa miradi ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea. 

Wakati huo huo, serikali, sekta ya biashara na wawekezaji nao bado hawajapunguza utoaji wa hewa chafuzi ili kutekeleza ahadi ya kuhakikisha kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi kwa mujibu wa mkabata wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, eneo ambalo Katibu Mkuu amesema nalo linahitaij kupaziwa sauti. 

Lengo hilo linamanisha kwamba nchi zinapaswa kuazimia kutotoa kabisa hewa chafuzi ifikapo katikati ya karne hii ya 21 na kuweka wazi mipango ya kufikia hatua hiyo. 

Mifano dhahiri 

Katibu Mkuu amepongeza serikali ya Italia ambayo kwa pamoja na Uingereza ndio wenyeviti wa COP26, kwa
“Mshikamano na madai yenu ya kutaka hatua zichukuliwe ni mfano dhahiri’ amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “tunahitaji viongozi wa kitaifa wafuate mfano wenu na wahakikishe wanafikia matokeo tunayohitaji katika COP26 na baada ya hapo.”