Kupiga makasia visiwani Tonga kunaonesha namna kulivyo na ukaribu baina ya wanadamu na bahari.

IFAD yawasaidia vijana nchini Tonga kupunguza unene na kupata ajira

UN World Oceans Day/Grant Thomas
Kupiga makasia visiwani Tonga kunaonesha namna kulivyo na ukaribu baina ya wanadamu na bahari.

IFAD yawasaidia vijana nchini Tonga kupunguza unene na kupata ajira

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tonga, moja ya mataifa ya visiwa vidogo lililoko katika bahari ya Pasifiki, vijana wanafundishwa stadi ya utengenezaji mitumbwi kama njia mojawapo ya kujipatia kipato, kulinda mazingira na kupunguza unene uliopitiliza au utipwatipwa.

Katika karakana ya utengenezaji wa mitumbwi nchini Tonga, taifa lenye visiwa vidogo 170 na ambako chakula si mazao yalimwayo nchini humo bali kwa kiasi kikubwa vilivyosindikwa na hivyo kusababisha kuwa moja ya nchi yenye watu wengi tipwatipwa duniani. 
 
Tawfiq El-Zabri ni Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD na anafafanua. 
"Tonga inakabiliwa na viwango vya juu kabisa vya lishe duni na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama unene kupita kiasi na mengi ambayo yanahusiana na ukosefu wa lishe bora. Eneo la ardhi ni dogo na limeathiriwa na maji ya chumvi, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la idadi ya watu na kwa hivyo ni muhimu watu hapa kupata nafasi ya kwenda baharini kuvua samaki. " 
 
Ili kunusuru vijana wa Tonga, IFAD ikaamua kuanzisha mradi kwa kushirikiana na serikali pamoja na taasisi ya MORDI TONGA ili kutoa mafunzo stadi ya kutengeneza mitumbwi, wakufunzi wakiwa ni wazee. 
 
Kupitia mafunzo mosi, vijana wanapata nyenzo za uvuvi, pili stadi za kupiga makasia zitawaweka kwenye afya njema kwani ni mazoezi, na tatu samaki watakaovua baharini watawasaidia si tu kupata kipato bali lishe bora kama anavyoeleza Alipate Sailosi mkufunzi na kiongozi wa jamii ya Eua. 
 
“Kwa sasa watu lazima walipe fedha ili waweze kwenda baharini kwa kutumia boti. Lakini ukiwa na mtumbwi, kisha ukapata kifungua kinywa kizuri, hapo kijana atapata nguvu ya kutosha kupiga makasia siku nzima ” 
 
Vijana walioanza kunufaika na mradi huu wa IFAD wanashukuru kama anavyosema Okusi Lama, “Nimejifunza vitu vingi wakati wa mafunzo. Ningependa kuwahimiza vijana wahudhurie kwa sababu hii inaweza kuwa njia ya kuwanufaisha sio tu kama wavuvi, bali pia kama mafundi. ” 
 
Mradi huo pia unakusudia kuwa hakikisho la upatikanaji wa chakula na kuwa chanzo cha kipato cha ziada kwa familia za Tonga.