Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa yu katikati ya ufukara, mkimbizi Yemen bado ana matumaini

Ibrahim Abdullah mkimbizi wa ndani nchini Yemen akiwa na binti yake Ghosson ambaye amekuwa akiugua utapiamlo
© UNICEF/Saleh Hayyan
Ibrahim Abdullah mkimbizi wa ndani nchini Yemen akiwa na binti yake Ghosson ambaye amekuwa akiugua utapiamlo

Ingawa yu katikati ya ufukara, mkimbizi Yemen bado ana matumaini

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Yemen maisha ya ufukara ni dhahiri miongoni mwa wakimbizi wa ndani ambapo hata kwa wale ambao walibahatika kupata vibarua, ajali kazini imeleta madhila na machungu zaidi na kuzidi kutia mashaka mustakabli wa watoto nchini humo

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa lakuhudumia watoto UNICEF inaonesha upepo unavuma katika kambi ya wakimbizi ya Al Shaheed jimboni Al Mukha nchini Yemen. Abdullah Jaber anarejea kwenye kibanda chake cha mabati akiwa na kile kitakachokuwa mlo wa siku kwa familia yake ya mke na watoto wawili. 

Analakiwa na mkewe Wardah ambaye anapokea kifurushi na kupeleka jikoni tayari kwa mapishi. 
Mazingira ya nyumba yao ni taswira halisi ya ufukara, malazi yamechakaa, halikadhalika vifaa vya jikoni. 

Abdullah akiwa anacheza na watoto wake Jaber mwenye umri wa miaka 3 na Ghosson binti huyu mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10, mkewe Wardah anaandaa mlo ambao ni viazi mbatata, karoti na biringanya. Kuni ni makaratasi na takataka.

Ibrahim Abdullah na familia yake wanaishi kwenye kambi nchini Yemen isiyo na paa, mvua yao jua lao.
© UNICEF/Saleh Hayyan
Ibrahim Abdullah na familia yake wanaishi kwenye kambi nchini Yemen isiyo na paa, mvua yao jua lao.

Baada ya muda mlo umeiva na kipaumbele ni binti yao Ghosson huku Jabber akiambulia kiduchu. Bwana Abdulla anasema, “awali hali yangu ilikuwa nzuri na niliweza kukimu familia yangu lakini nilipata ajali kazini na nimefanyiwa upasuaji mkononi, kwa hiyo nimeacha kufanya kazi hivyo sina kipato. Kuna nyakati mjomba wangu ananitumia fedha.” 

Familia hii ilihamia hapa kambini baada ya mapigano kuwafurusha kutoka jimboni Hudaydah. 
Baba huyu mwenye familia akaendelea na simulizi akisema, “nasikitika sana ninapokuwa sina fedha ya kuhudumia binti yangu, na wakati huo huwa natamani dunia ipasuke inimeze. Hata hivyo najitahidi na vile vile nahaha kusaka kibarua.” 

Ingawa yuko kwenye machungu, Bwana Abdulla katika video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF bado  ana matumaini, "natamani binti yangu Ghosson awe na afya njema kama watoto wengine na pia natumai atapata elimu nzuri siku za usoni.”