Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi maskini zaambulia patupu data za intaneti UNCTAD

Kundi la wasichana wa Namibia ambao walishiriki katika kambi ya mafunzo ya programu za Kompyuta (AGCC) mjini Pretoria, Afrika Kusini.
UN Namibia
Kundi la wasichana wa Namibia ambao walishiriki katika kambi ya mafunzo ya programu za Kompyuta (AGCC) mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Nchi maskini zaambulia patupu data za intaneti UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Uchumi wa kidijitali unaochochewa na data unazidi kushika kasi lakini wanaonufaka ni wakazi wa nchi tajiri ilhali wale walioko nchi maskini wakiendelea kuwa sehemu ya takwimu lakini si wachuma matunda.
 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo na Biashara, UNCTAD, ikipatiwa jina Ripoti ya Uchumi wa Kidijitali kwa mwaka 2021.

Makadirio yanaonesha kuwa mwenendo wa matumizi ya intaneti duniani utaongezeka mara tatu kati yam waka 2017 na 2022 huku janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 likiwa miongoni mwa sababu za ongezeko hilo kutokana na shughuli nyingi sasa kuhamia mtandaoni.

Mikondo ya usafirishaji wa intanenti imeongezeka kwa asilimia 35 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 26 mwaka uliotangulia wa 2019, imesema ripoti hiyo.

Ingawa hivyo mikondo iliyotumika zaidi ni kupitia vifaa vya mkononi kama vile simu za kiganjani au rununu ambapo ripoti inasema, “kutokana na ongezeko la vifaa hivyo vya kubebwa mkononi, mikondo ya kusafirisha intaneti inatarajiwa kuongezeka kwa takribani theluthi moja ifikapo mwaka 2026.”

Ripoti inaonesha kutokuwepo kwa usawa au kuwepo kwa pengo la kidijitali kati ya nchi tarjiri na maskini ambapo Mkurugenzi wa teknolojia UNCTAD Shamika N. Sirimanne anasema “kadri uchumi wa kidijitali unavokua, vivyo hivyo pengo la kidijitali.”

Mkimbizi kutoka DRC, Henriette Kiwele kiyambi akiandaa apu yake ya urembo katika karakana ya kuandaa apu kwenye kambi  ya wakimbizi ya Dzeleka nchini Malawi, ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuunganisha wakimbizi na intaneti unaofadhiliwa na UNHCR na Microsoft
UNHCR/Tina Ghelli
Mkimbizi kutoka DRC, Henriette Kiwele kiyambi akiandaa apu yake ya urembo katika karakana ya kuandaa apu kwenye kambi ya wakimbizi ya Dzeleka nchini Malawi, ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuunganisha wakimbizi na intaneti unaofadhiliwa na UNHCR na Microsoft

Nchi maskini ziko kando

Katika mwenendo huu mpya, nchi zinazoendelea ziko hatarini kusalia kuwa watoa data au sehmeu ya takwimu katika majukwaa ya kidijitali huku zikitakiwa kubeba gharama za taarifa za kiintelijensia zitokanazo na takwimu zao wenyewe.

“Ni asilimia 20 tu ya wakazi wa nchi zinazoendelea ndio wanaotumia intaneti, na hata wanapotumia, iko katika kasi ya chini mno na kwa gharama ya juu,” imetanabaisha ripoti hiyo.

Kama hiyo haitoshi, kasi ya intaneti katika nchi tajiri ni mara tatu zaidi  ya ile ya nchi zinazoendelea.
Halikadhalika wakati watu 8 kati ya 10 katika nchi tajiri wanafanya manunuzi mtandaoni, katika nchi zinazoendelea ni chini ya mtu 1 kati ya watu 10.

Mkondo wa kimataifa wa intaneti umejikita katika njia kuu mbili ambazo ni Amerika Kaskazini-Ulaya na Amerika Kaskazini-China.

Magwiji wa kidijitali nao wanazidi kujiimarisha

Majukwaa makubwa ya kidijitali ambayo ni Apple, Microsoft, Amazon, Alphabet (Google), Facebook, Tencent na Alibaba  nayo yanazidi kuimarisha minyonyoro ya thamani ya takwimu zao kote duniani.

“Wanawekeza katika ukusanyaji wa data kupitia majukwaa ya huduma kwa kutumia nyaya za meli aina ya nyambizi, setilaiti halikadhalika kuhifadhi data na kuzichambua kwa kutumia akili bandia au AI.”

Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018
IISD/ENB
Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018

Mfumo mpya wa usimamizi wa data unahitajika

Kwa kuwa mienendo ya data kuvuka mipaka inazidi kushamiri kupitia uchumi wa kidijitali, UNCTAD inataka mfumo mpya wa kusimamia mienendo hiyo duniani.

“Taasisi za sasa zinazoweza kuchukua na kukusanya data ziko katika nafasi nzuri ya kujinufaish ana takwimu hizo. Mfumo mpya wa kimataifa wa kusimamia mienendo ya data unahitajika ili manufaa ya data hizo yagawanywe kwa usawa,” amesema Bi. Sirimanne.

Vijana wenye vipaji wachukuliwa na nchi tajiri

Amesema dunia inapaswa kulipatia mtazamo sahihi pengo la sasa ambalo siyo tu ni kati ya nchi na nchi bali pia kampuni na mashirika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi maskini ziko hatarini kupoteza watu wao wenye vipaji katika sekta hiyo ambao wanachukuliwa na nchi tajiri, hali inayoweza kusababishwa zishindwe kuwa na uwakilishi thabiti kwenye mijadala ya kimataifa.