Watumishi wa WHO walitumia Ebola kudai ngono DRC: Dkt Tedros azungumza

28 Septemba 2021

Madai ya kwamba wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO walihusika na tuhuma za unyanyasaji wa kingono na ukatili wakati wa harakati za kukabili ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yanachukiza na ni usaliti dhidi ya watu tunaowahudumia.
 

Ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus aliyotoa leo Jumanne kufuatia matokeo ya ripoti ya tume huru iliyoteuliwa na shirika hilo kuchunguza madai ya uwepo wa matukio ya unyanyasaji wa kingono wakati wa mlipuko wa 10 wa Ebola nchini DRC.

Tume huru imebaini matukio 80 ya tuhuma za ukatili wa kingono wakati wa operesheni za WHO kudhibiti Ebola, matukio ambayo yanahusisha wafanyakazi 20 wa WHO. “Siku ya leo ni siku ya kiza kwa WHO na vitendo hivyo ni usaliti pia kwa wafanyakazi wenzetu ambao wanaweka maisha yao rehani kuhudumia watu wengine,” amesema Dkt. Tedros.

Uchunguzi ulianza lini?

Tume huru ya kuchunguza madai hayo ilianza kazi yake kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri mwezi Oktoba mwaka 2020.

Hii ni baada ya Ebola kutangazwa kutokomezwa kwenye maeneo hayo tarehe 25 mwezi Juni mwaka 2020, baada ya miaka miwili ya mlipuko wa gonjwa hilo katika eneo hilo lililogubikwa na mapigano.

Ebola ilisababisha vifo vya watu 2,300 na kutangazwa kuwa mlipuko wa pili kwa ukubwa zaidi duniani na hatari kuwahi kusababishwa na virusi.

Kulazimishwa kutoa mimba

Malick Coulibaly,  ambaye ni mjumbe wa jopo hilo, akizungumza wakati akiwasilisha ripoti ya kurasa 35 amesema walihoji makumi ya wanawake ambao walipatiwa kazi baada ya kukubali kutoa ngono.
Halikadhalika walihoji baadhi ya manusura wa ubakaji, ambapo visa 9 vilithibishwa.

“Wanawake waliohojiwa walisema watekelezaji wa vitendo hivyo hawakutumia njia za uzazi wa mpango na hivyo kusababisha baadhi ya wanawake kupata ujauzito. Baadhi ya manusura wamesema kuwa wanaume waliowabaka waliwalizimisha watoe mimba.” Amesema Bwana Coulibaly.

Watuhumiwa ni raia wa DRC na wa kigeni

Jopo limetambua watuhumiwa 83 wakiwa ni raia wa DRC na raia wa kigeni.Katika matukio 21, jopo liliweza kuthibitisha kuwa watekelezaji ni wafanyakazi wa WHO na wengi wao walikuwa raia wa DRC walioajiriwa kwa mikataba ya muda.

Watu hao wanatuhumiwa kutumia madaraka yao kuweza kutekeleza vitendo vya ngono.
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti, amesema “Shirika letu limeshtushwa na kuvunjika moyo kutokana na ripoti hii.”

Fikra za kukwepa sheria

Ripoti hiyo inasema kuwa kiwango cha ukatili na unyanyasaji wa kingono uliofanyika vimetokana na mazingira magumu waliyokuwa nao waliotendewa vitendo hivyo ambao hawakuwa wamepatiwa msaada wa kutosha na unaotakiwa katika mazingira kama hayo.

Uchelewashaji utoaji mafunzo kwa wafanyakazi pamoja na mameneja kukataa taarifa za tuhuma zilizotolewa kwa mdomo na udhaifu wa mifumo yalikuwa ni mambo yaliyobainika katika miji au vijiji 9 kwenye eneo hilo.
Wachunguzi pia waliona suala la wafanyakazi husika kujiona kuwa na uwezo wa kukwepa mkno wa sheria kwa vitendo dhidi ya manusura.

Umuhimu wa kurejesha imani

Kwa hali iliyotolewa, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros amesema watekelezaji na viongozi wote wanaotuhumiwa watachukuliwa hatua stahiki.

Akiomba radhi kwa manusura kutokana na machungu wanayoendelea kuyapata, Dkt. Tedros amesema anatambua fika umuhimu wa kujenga na kurejesha imani ya wananchi kwa WHO.

Lakini “kwa kuangazia udhaifu wa mtu mmoja mmoja na shirika, tunatumai kuwa manusura watahisi kuwa sauti zao zimesikika na hatua zimechukuliwa.” Ametamatisha Dkt. Tedros. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter