Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Punde ugonjwa wa uti wa mgongo utasalia historia, kulikoni?

Kampeni ya chanjo ya uti wa mgongo inafanyika huko Bouaké, nchini Côte d'Ivoire
© UNICEF/Frank Dejongh
Kampeni ya chanjo ya uti wa mgongo inafanyika huko Bouaké, nchini Côte d'Ivoire

Punde ugonjwa wa uti wa mgongo utasalia historia, kulikoni?

Afya

Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO na wadau wake wamezindua mkakati wa kwanza wa aina yake wa kutokomeza ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo, ugonjwa ambao unaua mamia ya maelfu ya watu kila mwaka. Mkakati huo, kwa mujibu wa WHO utaokoa maisha ya zaidi ya watu 200,000 kila mwaka. 

WHO kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema mkakati huo wa kutokomeza homa ya uti wa mgongo hususan ile inayosababisha na vimelea, itapunguza vifo kwa asilimia 70 na kupunguza kwa asilimia 50 wagonjwa.

Ukipatiwa jina, Mpango wa kimataifa wa kutokomeza homa ya uti wa mgongo ifikapo mwaka 2030, mkakati huo unalenga kuzuia maambukizi na kuboresha tiba na uchunguzi kwa wale ambao tayari wameambukizwa.

Akizungumzia ugonjwa huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk. Tedros Ghebreyesus amesema “popote pale ugonjwa huo unapotokea, unaweza kusababisha ulemavu au kifo. Unaingia haraka, una madhara makubwa kiafya, kiuchumi na kijamii na unasababisha mlipuko wenye madhara makubwa. Ni wakati wa kukabili homa ya uti wa mgongo duniani na kuitokomeza kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa chanjo, kusongesha tafiti na ubunifu, kubaini na kutibu aina zote za homa hii na kuimarisha huduma za usaidizi kwa wale waliougua ugonjwa huu.”

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, milipuko ya homa ya uti wa mgongo imeripotiwa katika kanda zote za dunia ingawa eneo lijulikanalo kama Ukanda wa Homa ya Uti wa Mgongo linalosambaa katika nchi 26 za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahari ndiko ulishamiri zaidi.

Mlipuko hautabiriki na unaweza kuathiri mfumo wa afya na kusababisha umaskini.

Tayari kuna chanjo kadhaa za kukinga dhidi ya homa ya uti wa mgongo lakini si jamii zote zenye uwezo wa kupata chanjo hizo na katika nchi nyingine bado chanjo hizo hazijajumuishwa katika programu za chanjo za kitaifa.

WHO na wadau wake wamesema watasaidia nchi kutekeleza mkakati huu ikiwemo kuandaa mipango ya kitaifa na kikanda ambayo itasaidia nchi kufikia malengo yao.

Homa ya uti wa mgongo ni ugonjwa hatari unaosababisha kuvimba kwa ngozi zinazonguka ubongo na uti wa mgongo na husababishwa na maambukizi yanayosababisha na vimelea na virusi.