Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urais si rahisi iwe kwa mwanaume au mwanamke – Rais Samia 

Rais Samia Suluhu Hassan akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili, jijini New York Marekani baada ya UNGA76. (23 Septemba 2021)
Ikulu Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan akihojiwa na Anold Kayanda wa UN News Kiswahili, jijini New York Marekani baada ya UNGA76. (23 Septemba 2021)

Urais si rahisi iwe kwa mwanaume au mwanamke – Rais Samia 

Wanawake

Rais Samia Suluhu Hassan akifafanua kuhusu usawa wa kijinsia katika uongozi na akianza kwa kujibu swali anavyoiangalia nafasi ya juu aliyonayo hivi sasa akiwa Rais wa Tanzania, anasema kazi hiyo si rahisi bila kujali jinsia. 

Kiongozi huyo mwanamke wa kwanza kukalia kiti cha urais katika nchi ambayo watangulizi wake sita wote walikuwa wanaume, ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa mara tu alipomaliza kuhutubia mjadala mkuu wa wazi wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York Marekani. 

Akijibu swali la mwanahabari Anold Kayanda wa Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa kuhusu iwapo anaona kuna uwezekano wa kufikia usawa wa kijinsia nchini Tanzania, Rais Samia anasema, «ni safari ndefu kufikia huko lakini mwelekeo upo. Na mwelekeo upo sio kwamba mimi nimeingia lakini kama tutakumbuka ukitazama kuanzia awamu ya nne tumekuwa tukielekeza kufikia usawa wa kijinsia. Ni awamu ya nne ile ile pia ambayo tulikuwa na bunge maalumu ambalo tulijadili katiba mpya ya Tanzania na ndani ya yale mapendekezo likaweko lile suala la hamsini kwa hamsini. Lakini pamoja na kwamba halijatoka kikatiba, utekelezaji unaendelea. Kwa mfano kwenye Bunge sasa hivi asilimia ya wanawake kushiriki ni kama asilimia 38 lakini Bunge lililopita tulikuwa kwenye asilimia 34 au 35. Kwa hiyo tumepanda mpaka 38. Na kwenye baraza la mawaziri, tulianza labda na asilimia 20 lakini mpaka uteuzi nilioufanya jusi, umetuvusha mpaka asilimia 36 na kazi inaendelea tutaweka wanawake wengi, pengine hatutafika hamsini kwa hamsini lakini tutasogea. Nilifanya uteuzi wa makatibu tawala wa mikoa na teuzi zilikuwa asilimia 46 kwa asilimia 54, asilimia 46 wanawake, 54 wanaume, kwa hiyo tunasogea. Wakuu wa wilaya hivyo hivyo hatukufikia 40 na kitu lakini tulikuwa kwenye 38 humo. Kwa hiyo tunakwenda polepole. Na imani yangu ni kwamba tutakapomaliza kipindi hiki cha miaka mitano, uchaguzi ujao, Tanzania tutakuwa na idadi kubwa ya wanawake.” 

Na kuhusu suala la anavyoichukulia nafasi au cheo cha urais alichonacho hivi sasa, Rais Samia anasema, “mimi nachukulia kwamba Tanzania tumepiga hatua kubwa. Kwa sababu kuwepo kwangu hapa kulianza na maamuzi ya makusudi kwamba kutekeleza ile hamsini kwa hamsini. Hamsini kwa hamsini tulikuwa tunisemea sana kwenye Bunge kwenda chini nafasi za madiwani na wengineo lakini mwaka 2015 serikali na Chama Cha Mapinduzi wakasema hapana hata juu kule tunakwenda hamsini kwa hamsini na ndio maana tukaamua ikiwa rais mwanaume, basi makamu wa rais atakuwa mwanamke, akiwa Spika mwanaume, Naibu Spika atakuwa mwanamke, na kinyume chake na pia nafasi nyingine. Sasa maamuzi yale ndiyo yaliyopelekea kuwa na Makamu wa rais wa kwanza mwanamke. Na katiba yetu inazungumza kwamba ikitokea sababu yoyote ile rais akashindwa kufanya kazi zake labda kwa sababu ya kifo, kuugua  au mambo mengine Makamu wa Rais atashika nafasi yake na ndivyo ilivyokuwa mimi nikawa Niko hapo, kuwa rais.” 

Nilitaka nihutubie UNGA76 kwa kutumia lugha ya Kiswahili - Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

 

Urais si jambo rahisi hata kwa mwanaume 

Kuhusu nafasi yake kama Rais Mwanamke, Rais Samia anasema, “kuwa na Rais mwanamke katika nchi za kiafrika si jambo rahisi. Na ikitokea kama ilivyotokea kwetu Tanzania, kuna maswali mengi watu wanajiuliza , je ataweza? Je, tutakuwaje? Na mkumbuke kwamba kwetu Rais ndiye Amir jeshi mkuu. Je anaweza akawa Amir jeshi mkuu? Je itakuwaje? Lakini kwa bahati nzuri, tumekwend vizuri. Tumekuwa na utaratibu mzuri wa kubadilishana, tumeingia vizuri tunaenda vizuri na kama mmesikia jusi tena nimefanya uteuzi nikavunja mwiko mwingine kwenye wizara ya ulinzi nikapeleka mwanamke na ni mwanamke ambaye si mwanamke tu ni mwanamke ambaye ana sifa anajua mambo ya ulinzi, amekaa kule SADC kwa miaka minane  na ndio yeye alikuwa anaangalia mamob ya ulinzi na usalama katika kanda yetu ile ya SADC kwa hiyo ni matumaini yangu atafanya kazi nao vizuri kwa kuwa anazijua hizo moja mbili tatu za sekta ya ulinzi.  Kwa hiyo si kazi rahisi. Si kazi rahisi hata kwa mwanaume. Kwa sababu nilikuwa namwona Rais, marehemu rais John Pombe Magufuli alivyokuwa akihangaika na mimi nilikuwa msaidizi wake wa karibu. Ukiwa waziri huku huwezi kuona vizuri kinachoendelea lakini ukiwa makamu wa rais unamuona rais anavyohangaika kwa hivyo si rahisi hata kwa mwanaume. Kwa hiyo kwa mwanamke inaongezeka ile imani ya watu. Je wanakupa imani yao?.”  

Mama anaupiga mwingi 

Rais Samia akifafanua kuhusu imani ya watu kwa rais mwanamke anasema, “lazima ufanye sana wakuone ndio wakupe imani , magazeti yaandike, ‘Mama kaupiga mwingi ndio watu  watu wanakupa imani, sijui mama kafanya nini huko, ndio watu wanarudisha imani. Kwa hivyo ni kazi kidogo.”