Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utalii katika zama za COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi :UNWTO

Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.
TTB Video screenshot
Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.

Utalii katika zama za COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi :UNWTO

Ukuaji wa Kiuchumi

Hamu ya kusafiri na kujionea ulimwengu bila ya ubaguzi ni tabia ya watu wote, na kwa hivyo utalii unapaswa kufungua mlango kwa kila mtu na kila mtu anapaswa kuweza kunufaika na faida zake za kijamii na kiuchumi limesema shirika la utalii la Umoja wa Mataifa duniani WTO. 

Katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya utalii hii leo ambayo imebeba mada “utalii kwa maendeleo jumuishi” siku inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 27,  Zurab Pololikashvili, katibu mkuu wa UNWTO amesema “Sekta ya utalii inaajiri mtu mmoja kati ya watu kumi duniani. Kukatizwa kwa safari za kimataifa kulikosababishwa na janga COVID-19 kumedhihirisha wazi jinsi utalii ulivyo muhimu kwa jamii zetu,"  

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amesema “Sekta ya utalii bado inakabiliwa na hasara kubwa kutokana na janga la COVID-19. Katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu, mtiririko wa watalii wa kimataifa katika sehemu nyingi duniani ulipungua kwa asilimia 95, na ajira milioni 100 hadi milioni 120 zilikuwa hatari.” 

Wakati huo huo, kwa mujibu wa utabiri, hadi mwisho wa 2021 ujazo wa pato la taifa utapungua kwa zaidi ya dola trilioni 4. "Kwa nchi zilizoendelea hii ni mshtuko mkubwa, lakini kwa nchi zinazoendelea ni hali ya dharura," ameongeza Katibu Mkuu Guterres. 

Masikini ndio waathirika zaidi 

Bwana Guterres, amebainisha kuwa sekta ya utalii imeunganishwa na karibu nyanja zote za uchumi na sekta za jamii, lakini sio kila mtu anayeweza kutumia  na kunufaika na faida zake.  

Kwa upande mwingine, mgogoro wa utalii kama huu wa sasa ameongeza unagonga na kuathiri zaidi makundi duni na yaliyo hatarini tangu mwanzo.  

“Ndio maana mwaka huu kaulimbiu ya siku ya siku ya mwaka huu ni wito wa maendeleo shirikishi ya sekta ya utalii.” amesisitiza 

Kulingana na mkuu wa shirika la utalii duniani Zurab Pololikashvili, "faida za ukuaji wa utalii zinapaswa kuhisiwa katika ngazi zote za sekta yetu kubwa na yenye njanja mbalimbali, kuanzia kwenye mashirika makubwa ya ndege hadi biashara ndogo zaidi za familia." 

Jumba la kumbukumbu la Uingereza, London lilifunguliwa tena katika msimu wa joto na vizuizi vya COVID-19 vimewekwa
IMF/Jeff Moore
Jumba la kumbukumbu la Uingereza, London lilifunguliwa tena katika msimu wa joto na vizuizi vya COVID-19 vimewekwa

COVID-19, utalii na taka za plastiki 

Mbali na janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya utalii amesema Katibu Mkuu. 

Nchi za visiwa vidogo zimeathirika zaidi, ambapo utalii huchukua karibu asilimia 30 ya shughuli za kiuchumi.  
Wakati huo huo, njia sahihi ya kujikwamua na kukuza sekta ya utalii, anasema Guterres, kunaweza kutoa kazi nzuri na kukuza uchumi jumuishi, faida ambayo inaweza kufurahiwa na wanajamii wote. 

"Hii inahusu hatua inayolenga uwekezaji kuelekea utalii unaojali mazingira ambao unamaanisha kutokuwamo kwa hewa ukaa katika sekta zenye uzalishaji mwingi, ikiwemi sekta ya anga, bahari na huduma," ameelezea António Guterres. 

Njia moja ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira ni mradi wa UNWTO wa kukabiliana na taka za plastiki na uchafuzi wa mazingira ambao kampuni kadhaa tayari zimejiunga na idadi inaongezeka. 

"Kutatua changamoto ya taka za plastiki ni muhimu sana kwa kurejesha utalii kuwa rafiki wa mazingira, na kuhifadhi maeneo maarufu kwa watalii, na kuzuia mabadiliko ya tabianchi," anasema Zurab Pololikashvili. 

Na mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anasisitiza kuwa ni kwa kufanya tu maamuzi ambayo yanazingatia masilahi ya raia wote, tutaweza kutambua uwezo wa utalii "kama nguvu ya ustawi, njia ya ujumuishaji, chombo cha kulinda sayari yetu na bioanuwai na sababu ya uelewa wa tamaduni miongoni mwa watu. "