Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN ikitaka kuendelea kuwa na manufaa inapaswa kuboresha ufanisi wake na kuweza kutegemewa:India 

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akihutubia mjadala wa Baraza Kuu wa UN UNGA76
UN Photo/Cia Pak
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akihutubia mjadala wa Baraza Kuu wa UN UNGA76

UN ikitaka kuendelea kuwa na manufaa inapaswa kuboresha ufanisi wake na kuweza kutegemewa:India 

Masuala ya UM

Waziri mkuu wa India Narendra Modi ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo katika mjadala mkuu wa wazi wa UNGA76 kuwa wakati India inafanya mageuzi, ulimwengu hubadilika. 

Akiwa mzungumzaji wa kwanza katika mjada huo wa leo Jumamosi Modi amegusia masuala mbalimbali ya muhimu kwa taifa lake na jumuiya ya kimataifa ikiwemo ujumuishi katika masuala ya demokrasia nchini mwake na umuhimu wake kote duniani lakini pia ameeleza jinsi gani mageuzi nchini India yanavyoweza kusaidia kuleta mabadiliko duniani kote. 

"Wakati India inakua, ulimwengu unakua, wakati India inabadilika, ulimwengu hubadilika. Maendeleo yanapaswa kujumuisha wote, kuwa na lishe bora, kugusa kila kitu na kuenea kila mahali. Hiki ndicho kipaumbele chetu," ameongeza. 

Waziri Mkuu Modi pia amezungumzia juu ya shida iliyopo ya upatikanaji wa maji ya kunywa ulimwenguni kote, ikiwemo India.  

"Maji machafu sio shida tu nchini India ni shida kubwa katika nchi masikini na zinazoendelea pia," amesisitiza Waziri mkuu huyo na kuongeza "Ili kukabiliana na changamoto hii, tunaendesha kampeni kubwa ya kuunganisha kaya 17  kila mtaa na mabomba ya maji safi." 

Chanjo ya COVID-19 

 Wakati huo huo, katika hotuba yake waziri mkuu Modi amewaalika watengenezaji wa chanjo duniani kwenda India. 

"India imekuwa nchi ya kwanza kutengeneza chanjo inayotegemea DNA ambayo inaweza kuchukuliwa na mtu yeyote ambaye ana zaidi ya miaka 12.” 

Pia amewaenzi watu wote waliopoteza maisha kutokana na janga la COVID-19 na kutoa pole kwa familia za wafiwa na wanaoendelea kuuguza wagonjwa wa janga hilo. 

Masuala mengine aliyoyapa kipaumbele katika hotuba yake ni mabadiliko ya tabianchi, ushirikiano wa kimataifa, masuala ya usawa wa kijinsia na mabadiliko katika Umoja wa Mataifa ambapo amesema “Endapo Umoja wa Mataifa unataka kuendelea kuwa na manufaa ni lazima uboreshe ufanisi wake na kuweza kutegemewa.”