WHO yaruhusu Regeneron itumike kutibu COVID-19, kampuni zatakiwa kupunguza bei

Hatimaye shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limeidhinisha matumizi ya Regeneron ambayo ni mchanganyiko wa dawa aina ya Casirivimab na Imdevimab unaotumika kutibu watu wenye ugonjwa wa Corona au COVID-19.
Hatua ya WHO imetangazwa hii leo huko mjini Geneva, Uswisi na Dkt. Janet Diaz kutoka Idara ya utatibu huku akisema “tunatoa wito kwa gharama ya Regeneron ipunguzwe sambamba usambazaji wake uwe sawia.”
“Hii ni hatua kubwa sana,” amesema Dkt. Diaz akiongeza “ni pendekezo letu la kwanza kwa ya tiba kwa wagonjwa wenye dalili za kati au zisizo kali za COVID-19 kwa sababu inapunguza uhitaji wa mgonjwa kulazwa iwapo huko kwenye hatari zaidi.“
Hii ina maana kwamba dawa hii inapendekezwa kutumika kwa wagonjwa ambao si wagonjwa mahututi lakini wako katika hatari ya kuweza kulazwa hospitalini kutokana na COVID-19 au wale ambao wana dalili kali za ugonjwa huo na hawana kinga ya kutosha mwilini.
“Kwa kuwapatia kinga nyongeza ya mwili kwa wagonjwa hao kumeonesha kuleta majibu mazuri, na faida yake ni nini? Tunapunguza vifo,” amefafanua Dkt. Diaz wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva hii leo.
Tiba hiyo ya kuongeza kinga ilipatiwa ruhusa ya matumizi ya dharura nchini Marekani mwezi Novemba mwaka jana baada ya kutumiwa kumtibu aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo Donald Trump baada ya kulazwa hospitali alipougua COVID-19.
Uingereza nayo imeshaidhinisha matumizi ya Regeneron, ilhali Muungano wa Ulaya bado unaifanyia tathmini.
Hatua ya WHO kuidhinisha dawa hiyo inazingatia matokeo kutoka utafiti uliofanyika nchini Uingereza kwa wagonjwa 9,000 waliotumia dawa hiyo na kudhihirisha kuwa inapunguza vifo kwa wagonjwa waliokuwa wamelazwa hospitali na ambao kinga zao za mwili zilishindwa kukabiliana na virusi.
Dawa hiyo imekuwepo sokoni kwa miongo kadhaa kutibu magonjwa mengine kama vile saratani na msingi wake inatoa vikinga mwili vinavyofanana na vile vinavyozalishwa na mwili ili kupambana na maambukizi.
Kampuni ya Roche ya Uswisi imekuwa inatengeneza dawa hiyo kwa ushirikiano na kampuni ya Regeneron inayomiliki hataza ya dawa hiyo.
Dkt. Diaz amesihi kampuni ya Regeneron kupunguza bei na iangalie uwezekano wa usambazaji kwa uwiano duniani kote.
WHO inasema “Tunafahamu faida za kuokoa maisha kwa wagonjwa wa COVID-19 ni dhahiri na zitahitaji hatua. UNITAID ambalo ni shirika tanzu la WHO la kusaka dawa kwa bei nafuu linawasiliana na ROCHE ili ipunguze bei na kuweka mgao sawia wa dawa hizo duniani kote ikiwemo nchi za kipato cha chini na kati.”