Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa upandaji miti wanufaisha wakimbizi nchini Cameroon

Wakimbizi huko Minawao, kaskazini mashariki mwa Kamerun, wanapanda miti katika mkoa ambao umekatwa misitu kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu.
© UNHCR/Xavier Bourgois
Wakimbizi huko Minawao, kaskazini mashariki mwa Kamerun, wanapanda miti katika mkoa ambao umekatwa misitu kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za kibinadamu.

Mradi wa upandaji miti wanufaisha wakimbizi nchini Cameroon

Tabianchi na mazingira

Mradi kabambe wa upandaji miti, ulioanzishwa mwaka 2018 katika kambi ya wakimbizi ya Minawao nchini Cameroon kwa ushirikiano kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR na shirikisho la waluteri duniani, LWF umesaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzuia kuenea kwa jangwa katika ukanda wa Sahel. Leah Mushi ana taarifa zaidi kutoka katika video ya UNHCR.

Taswira mbili tofauti kutoka angani za eneo kame la kambi ya Minawao mwaka 2018 na eneo lenye  ukijani mwaka huu wa 2021.

Eneo hili ni makazi ya wakimbizi wa ndani zaidi ya 70,000 walioyakimbia makazi yao ya asili kutokana na vurugu za kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kuanzia mwaka 2014.

UNHCR kwa kushirikiana na shirikisho la kiluteri duniani, LWF walianzisha mradi maalum wenye lengo la kupanda miti, kupunguza ukataji miti na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kati ya mwaka 2018 mpaka 2021 zaidi ya miche 360,000 imepandwa katika eneo la ukubwa wa hekta za mraba zaidi ya 100 na Lydia Youcoubou, mkimbizi na mfanyakazi wa kitalu cha miche anasema, “Minawao imekuwa mahali ambako ni kijani kibichi kote, na kuna faida nyingi tunapata. Tuna kivuli, udongo umekuwa na rutuba na miti inaleta maji.”

Kwa upande wake Abdul Aziz, mratibu wa Mradi wa LWF anasema mradi umekuwa na mafanikio makubwa. "Hatujaelekeza nguvu zetu kwenye kutoa elimu na kupanda miti pekee. Tumefanikiwa kuondoa changamoto ya utakaji miti, tumeanzisha mkakati kwa kushirikiana na UNHCR wa kuhamasisha vyanzo mbadala vya nishati kama matumizi ya mkaa usiotokana na miti ambao ni rafiki wa mazingira."

Mradi huu unaogharimu zaidi ya dola milioni 2.7 ni sehemu ya mradi ujulikanao kama “Ukuta mkubwa mzuri wa Kijani” ulioanzishwa barani Afrika ukikusudia kupanda miti barani Afrika kwenye eneo la ukubwa wa Kilometa za mraba 8,000 na kuzuia kuenea kwa jangwa katika ukanda wa Sahel.