Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenyatta aeleza vipaumbele vyake Kenya itakapotwaa urais wa Baraza la Usalama la UN 

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 kwa njia ya video.
UN Photo/Cia Pak
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 kwa njia ya video.

Kenyatta aeleza vipaumbele vyake Kenya itakapotwaa urais wa Baraza la Usalama la UN 

Amani na Usalama

Kenya ikiwa tayari kukalia kiti cha urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Oktoba, Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta kupitia hotuba yake kwenye UNGA76 ameeleza vipaumbele vyake. 

Bwana Kenyatta akizungumza kutoka katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya kupitia hotuba iliyorekodiwa, amelieleza Baraza la Umoja wa Mataifa kwamba anaamini mifumo ya ushirikiano wa kimataifa inapaswa kuwa ya haki, inayojumuisha na yenye ufanisi. 

“Ulimwengu unapaswa kutilia maanani onyo alilolitoa Katibu Mkuu.” Ameeleza Bwana Kenyatta akirejelea ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwamba ubinadamu unakabiliwa na chaguo la dharura, kushinda au kushindwa na hivyo kusisitiza uwepo wa hatua za pamoja kwa ushirikiano wa kimataifa katika kutatua changamoto za ulimwengu. 

Kenyatta amesema amepanga kuongoza matukio kadhaa wakati Kenya ikiongoza ambapo masuala hayo ni pamoja na kufanya utofauti kuwa lengo kuu katika ujenzi wa taifa, kuchunguza athari za silaha ndogo ndogo haramu na silaha nyepesi kwa operesheni za ulinzi wa amani na pia usaidizi ulio bora kwa walinda amani wanawake na wajenzi wa amani. 

Pia Kenyatta ametangaza kuwa Kenya iko tayari kiongozi wa uchumi kijani. Amesema Afrika inayokua haraka inaweza kutoa kwa ulimwengu wote faida ya gawio la wananchi wake vijana na fursa za uwekezaji. Uhuru Kenyatta amepigia debe ushiriki wa Kenya katika mikutano ya bahari akisema, "tunatazamia kuwa wenyeji wa mkutano wa pili wa bahari, kwa kushirikiana na ureno mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2022 kwa ajili ya kutekeleza ahadi za ushirikiano ambazo zitahamasisha matamanio ya hatua ya kimataifa ya bahari na kuongeza uwekezaji katika uchumi wetu wa buluu.”  

Akigusia suala la usalama, Kenyatta amesema kuwa mataifa hayana uwezo wa kukabiliana na udhaifu unaosababisha mizozo na ugaidi. Kwa hivyo ni muhimu kuongeza uwezo wa mataifa kusimamia tofauti za kijamii na kisiasa.  

Na kuhusu ugonjwa wa Covid-19 Rais Kenyatta amesema hadi kufikia wiki iliyopita zaidi ya wakenya 5000 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Corona, na akaongeza kusema, “tunawaomboleza wakenya hawa pamoja na zaidi ya zaidi watu milioni 4.7 ambao wamefariki dunia kote duniani.”  

Aidha ameeleza kuwa vizuizi vya Covid-19 vimeathiri sana uchumi na wakati wa kujijenga upya kurejea katika hali ya kabla ya Covid-19 ni sasa na njia ya kufika hapo ni kupitia chanjo kwa wote, na kwa usawa inagawa, “bahati mbaya hali haiku hivyo hivi sasa.”  

TAGS: UNGA76, Uhuru Kenyatta, Kenya