Hakuna aliye na haki ya kumbagua mwingine sababu ya rangi yake:Mongella

22 Septemba 2021

Wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 76 #UNGA76 leo likijikita na mjadala wa ngazi ya juu kuadhimisha miaka 20 tangu kupitishwa kwa azimio la Durban linalopinga ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina zingine, imeelezwa kwamba hatua zimepigwa katika kupambana na ubaguzi wa rangi lakini bado kuna kibarua kigumu cha kufikia lengo la kutokomeza kabisa ubaguzi huo katika Nyanja mbalimbali.

Mkutano huo wa ngazi ya juu unajumuisha nchi wanachama 193 na wadau wengine wa masuala ya haki za binadamu umebeba mada “malipo, haki ya kijamii na usawa kwa watu wenye asili ya Kiafrika” unatathimini hatua zilizopigwa, mafanikio na changamoto ambazo bado zipo kukabiliana na jinamizi hilo duniani.  

Katika hotuba yake kwenye mjadala huo wa wazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ubaguzi wa rangi na ubaguzi mwingine umekuwa kama donda ndugu kila pembe ya dunia na hivyo “Ninatoa wito kwa kila nchi mwanachama kuchukua hatua madhubuti pamoja na kupitisha hatua za kisera,sheria na ukusanyaji wa takwimu ili kuunga mkono juhudi zote za kitaifa na Kimataifa za kupambana na janga hili.” 

Dkt. Getrude Mongella aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuundwa kwa azimio hilo miaka 20 iliyopita akizungumza na Stella Vuzo wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa UNID Dar es salaam nchini Tanzania kuhusu tathimini hiyo anasema  

“Hapa Tanzania tumeweza kuchukua hatua za kuwalinda albino lakini huko nje bado katika sehemu nyingine hasa wale wanaobagua watu Weusi kwamba hali haijawa nzuri. Mimi nakumbuka nilipokuwa naongoza mkutano wa Beijing kuna wakati nikitembelea baadhi ya nchi ambazo sizitaji unafika mahali wanasema leteni pasispoti tuone, wale weupe wanapitishwa tu kwenye msitari na mpaka sekretari wangu alipitishwa, sisi wengine weusi tunazuiliwa na alikuwa ameaibika kabisa nikamwambia ndio dunia ilivyo, ya kwamba wewe unafikiriwa ni wajuu kwa sababu ni mweupe, na mimi kwa sababu ni mweusi hawajui nina cheo kikubwa kuliko wewe. Hivyo ubaguzi wa rangi bado upo na sidhani utaisha tu kama serikali zetu hazisaidii kuchukua hatua za dhati” 

Je nini kifanyike kuhakikisha ubaguzi huo unatokomezwa? 
“Sheria za nchi ziwe kali zaidi, zitekelezwe zaidi dhidi ya ubaguzi wa rangu kuliko familia, kwa sababu mazingira ambamo wanakutana watu wa rangi mbalimbali sio mazingira ya kawaida ndani ya famialia. Wazazi wana nafasi wakati wote katika kuondoa fikra ambazo si sahihi ndani ya jamii. Inaweza kabisa ikaweka kwenye mafundisho ya vijana wetu, muhitasari ya elimu ili mtoto anapofundishwa angali mdogo kuona ubaya wa kubaguana sababu ya rangi, ni kitu ambacho kiukweli kinatuharibia raha ya kuishi pamoja kama binadamu na tusipokuwa na sheria zinazodhibiti hatuwezi tukauondosha utachukua muda mrefu” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter