Lishe duni kwa watoto bado ni mtihani mkubwa duniani- UNICEF

22 Septemba 2021

Watoto wenye  umri wa chini ya miaka 2 hawapatiwi chakula au virutubisho wanavyohitaij ili waweze kukua vyema na hivyo kukwamisha makuzi yao, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF hii leo.

Katika Video iliyotolewa na UNICEF inaonesha taswira ya lishe kwa watoto ikianzia Indonesia mama na mwanae mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja akichagua matunda sokoni na kisha mlo kamiliifu wa wali, mboga na kitoweo akipatiwa mtoto.

Kisha ni Sudan Kusini katika kituo cha afya ya mama na mtoto kazi ikiwa ni upimaji wa viwango vya utapiamlo.

Ripoti ya UNICEF ikipatiwa jina la Wamelishwa ili Wakwame? Janga la mlo watoto wakiwa wachanga, imetolewa leo wakati kunafanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mifumo endelevu ya chakula.

Ripoti inaonya kuwa ongezeko la umaskini, ukosefu wa usawa, mizozo, majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, na dharura za afya kama vile janga la COVID-19 vinasababisha janga la lishe miongoni mwa watoto na hakuna dalili zozote za mabadiliko katika miaka 10 iliyopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore anasema, “Matokeo ya ripoti hiyo ni dhahiri kwamba hali inapokuwa mbaya, mamilioni ya watoto wanalishwa mlo waporomoke. Lishe duni katika miaka miwili ya mwanzo ya mtoto inaweza kukwamisha ukuaji wa viungo na ubongo na hivyo kuwa na madhara yasiyorekebishika kielimu, ajira na mustakabali wake. Wakati tumebaini hilo kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwepo na maendeleo kidogo katika kuwapatia watoto lishe bora na salama. Na COVID-19 inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.”

Uchambuzi uliofanyika katika nchi 91 umebaini kuwa ni nusu tu ya watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi 23 ndio wanapatiwa idadi ya milo inayotakiwa kwa siku, huku theluthi moja wanapatiwa kiwango kidogo cha mlo ili waweze kuishi.

Janga la COVID-19 limefanya hali kuwa mbayá zaidi kwa kuwa baadhi ya familia zimelazimika kupunguza ununuzi wa vyakula vyenye lishe kutokana na ukata.

Ripoti inapendekeza kuwa ili watoto wapate lishe bora, serikali, wahisani, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo washirikiane kubadili mifumo ya vyakula, afya, hifadhi ya jamii kwa kuchukua hatua kama vile kuongeza fursa ya kupata na kumudu vyakula vyenye lishe yakiwemo matunda, mboga za majani, mayai, nyama, Samaki na vile vilivyoongezewa virutubisho kwa kuwekea motisha uzalishaji, usambazaji na uuzaji wake.

Halikadhalika kutekeleza sheria na kanuni za kitaifa za kulinda watoto dhidi ya vyakula visivyo na lishe na kutokomeza mbinu hatarishi za kibiashara zinazolenga watoto na familia zao.

Mbinu mbalimbali za mawasiliano zitumike kuhamasisha matumizi ya vyakula salama na vyenye lishe ili wazazi na watoto waweze kutambua umuhimu wa vyakula hivyo. Ripoti inasema hilo linawezekana kwa kuwekeza.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter