Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Accra kuwa mji mkuu wa dunia wa vitabu mwaka 2023

Duka la vitabu huko Yangon, Myanmar
Unsplash/Alexander Schimmeck
Duka la vitabu huko Yangon, Myanmar

Accra kuwa mji mkuu wa dunia wa vitabu mwaka 2023

Utamaduni na Elimu

Mji mkuu wa Ghana, Accra umetangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuwa mji mkuu wa dunia wa vitabu kwa mwaka 2023.

Taarifa ya UNESCO iliyotolewa Paris, Ufaransa hii leo imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Audrey Azoulay akisema kuwa hatua hiyo inazingatia tathmini ya kamati ya ushauri ya miji ya vitabu ya dunia baada ya kupitia andiko la Accra la kupanua wigo wa usomaji vitabu.

Mpango wa Ghana unatambua jinsi vitabu vinavyoweza kuleta mabadiliko ya kitamaduni na utajiri wa Ghana kupitia watoto na vijana na hivyo kujenga kizazi kijacho chenye stadi thabiti.

Watakaojumuishwa kwenye mpango huo ni makundi yaliyo pembezoni yenye kiwango cha juu cha kutokujua kusoma na kuandika wakiwemo wanawake, vijana, wahamiaji, watoto wanaozurura mitaani na watu wenye ulemavu.

Sherehe zitaanza tarehe 23 mwezi Aprili mwaka 2023 ambayo ni siku ya vitabu na hakimiliki duniani.

Mkakati wa utekelezaji unajumuisha kusambaza vitabu vya kusoma ili kujenga tabia ya kusoma vitabu ambapo pia sekta ya uchapishaji vitabu nayo inapatiwa hamasa na Accra inatumia mbinu mbalimbali za kuhamasisha kusoma kwa kuanzisha pia maktaba tembezi sambamba na kufanyika kwa warsha za kuhamasisha uandishi wa vitabu kwa lugha mbalimbali za Ghana.

Andiko la Ghana kuweza kupata hadhi pia liligusia pia uhuru wa mtu kupata taarifa ikiwa ni kuelekea siku ya uhuru wa vyombo vya Habari mwaka 2023.

Accra inakuwa jiji la 23 kupata hadhi hiyo tangu kuanzishwa kwa tukio hilo mwaka 2001. Miji mingine ya Afrika iliyowahi kupata hadhi hiyo ni Port Harcourt Nigeria mwaka 2014 na Conakry Guinea mwaka 2017.