Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makamu wangu wa Rais, Spika na Naibu Spika wa Bunge wote ni wanawake-Rais Hichilema wa Zambia 

Rais Hakainde Hichilema wa Zambia akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76
UN Photo/Cia Pak
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76

Makamu wangu wa Rais, Spika na Naibu Spika wa Bunge wote ni wanawake-Rais Hichilema wa Zambia 

Wanawake

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema akihutubia kwa mara ya kwanza mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76, pamoja na kusisitiza masuala mengine kama uhusiano wa kimataifa, amani, Covid-19 na mabadiliko ya tabianchi, ameeleza mkakati wake wa kuinua usawa wa kijinsia katika nchi yake. 

Bwana Hichilema ambaye ni Rais Zambia kuanzia tarehe 24 mwezi uliopita yaani Agosti 2021 amechaguliwa kuiongoza nchini hiyo akiwa ni Rais wa 7 akipigia chepuo haki za wanawake amesema wito wa usawa wa kijinsia hivi sasa ni mapambano ya yaliyodumu kwa karne kwa ajili ya wanawake kushiriki saw ana wanaume katika jamii.  

“Licha ya kutambua kuwa ushiriki kamili wa wanawake katika maeneo yote ya maisha unasaleta mafanikio, wanawake bado hata hivyo wameshiriki kwa kiasi kidogo katika maisha ya umma na katika kufanya maamuzi.” Amesema Rais Hichilema. 

Rais Hichilema ameendelea kuelezea kwamba ni muhimu kuendelea kutaka kuhamasisha usawa wa kijinsia na hususani msisitizo ukiwekwa ukiwekwa katika haki ya wanawake, wasishana, watoto na haki za wanaoishi na ulemavu.  

Akieleza hatua ambazo tayari wameanza kuzichukua, Raisa Hichilema amesema, “kwa sisi Zambia, tutasalia katika kuendeleza na kukuza haki za wanawake na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Bunge letu jipya limemchagua Spika wake wa kwanza wa kike kuongoza mhimili mkuu wa utungaji sheria Zambia.” Kisha akaongeza akisema, “ninatamani pia kueleza kwa Fahari kwamba Makamu wa Rais wa Zambia na pia Naibu Spika wa Bunge ni wanawake.” 

Vilevile Rais Hichilema amesema Sambamba na kujitolea kwao, Zambia inatekeleza mikakati mbalimbali iliyobuniwa inayowalenga wanawake na vijana ili kuwainua kiuchumi Akieleza kuwa, “wakati wa kuyafanya haya yote lengo letu ni kuondoa njaa na umaskini vijijini.”  

Covid-19 na chanjo 

Kuhusu Covid-19 Rais Hichilema ameeleza namna nchi yake kama zilivyo nchi nyingine imeathirika kiuchumi na Covid-19 na kwamba moja ya mbinu za kupambana na ugonjwa huu ni chanjo lakini hadi sasa Zambia imeweza kuwachanja asilimia 3 tu ya watu wote wenye sifa za kuchanjwa ingawa lengo lilikuwa kuwachanja angalau asilimia 70 na hivyo kutoa rai kwa jumuiya ya kimataifa kulitupia jicho bara la Afrika ikizingatiwa kuwa hadi kufikia sasa chanjo zimeshatolewa zaidi ya bilioni mbili kote duniani lakini Afrika bado sana kufikia lengo.