Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 imezidisha pengo la ujira kati ya wanawake na wanaume

Ujira kwa wanawake wafanyakazi bado ni changamoto
ILO/A. Khemka
Ujira kwa wanawake wafanyakazi bado ni changamoto

COVID-19 imezidisha pengo la ujira kati ya wanawake na wanaume

Masuala ya UM

Hii ni leo ni siku ya kimataifa ya usawa katika ujira ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la ugonjwa wa  Corona au COVID-19 limezidi kupanua pengo la ujira lililokuwepo hata kabla ya ugonjwa huo.

Katika ujumbe wake wa siku hii ya leo, Bwana Guterres amesema kabla ya COVID-19 wanawake walikuwa hawapati ujira kwa kazi wanayofanya ya maleziya watoto na watu wengine katika familia ambao hawawezi kujitunza wenyewe.

“Janga la COVID-19 limelazimu huduma ya malezi ya watoto na watu hao wazima kuenguliwa kutoka katika mazingira ya kawaida na kurejeshwa nyumbani na hivyo kuongeza pengo la ujira. Wanawake wengi wanahaha kuhakikisha wanabakia na ajira zao huku wakilea watoto, wakihusika na elimu ya watoto wao kwa njia ya mtandao,  kutunza wagonjwa au wanafamilia bila hata ujira wowote,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amesema kuwekeza katika sekta ya malezi ya jamii kunasaidia kupunguza pengo la ujira kwa kufungua ajira mpya huku ikiwaondoa wanawake katika mazingira ya kufanya kazi bila ujira na badala yake kupata ajira rasmi.
 
Amekumbusha kuwa katika sekta ya afya nako, wengi walio mstari wa mbele katika kutoa huduma ni wanawake. “Mara nyingi ujira wao ni mdogo kuliko wanaume, hawana uwezo wa kupitisha maamuzi na wako hatarini zaidi kukumbwa na ukatili na manyanyaso.”
 
Akirejelea mazungumzo yake na mhudumu mmoja wa afya nchini Ghana aitwaye Scholastica Dery, Katibu Mkuu anasema “nilikumbushwa kwa dhati juu ya majukumu mawili ya mwanamke nilipozungumza naye akisema kama mfanyakazi niliye mstari wa mbele sisi ni wengi. Ukijumuisha jukumu  hili na majukumu yetu ya nyumbani si rahisi, lakini tumeazimia kufanya kazi hii.”
 
Guterres amesema licha ya kuwepo kwa sheria za ujira sawa, wanwaake wanalipwa wastari wa senti 80 ya kila dola moja anayolipwa mwanaume kwa kazi inayofanana “takwimu ni ya chini zaidi kwa watu wa asili ya Afrika na wale wenye watoto.”

Amesema kushughuliia janga la COVID-19 kunatoa fursa ya kipekee y kuandika makubaliano mapya ya kijamii ambayo yanazingatia haki za wanawake ikiwemo zile za ujira sawa na kwamba, “hili ni jambo la haki na wajibu kwetu sote.”

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema katika siku ya leo ya kimataifa ya ujira sawa, “hebu na tuazimie kuvunja ubaguzi na fikra potofu za kijinsia ambazo zinasababisha kuwepo kwa pengo la ujira kijinsia.”