Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha za IMF kuwezesha Tanzania kujenga viwanda vidogo 7 vya hewa tiba ya oksijeni

Mitungi ya oxijeni kwa ajili ya tiba hospitalini
Morning Brew on Unsplash
Mitungi ya oxijeni kwa ajili ya tiba hospitalini

Fedha za IMF kuwezesha Tanzania kujenga viwanda vidogo 7 vya hewa tiba ya oksijeni

Msaada wa Kibinadamu

Tanzania imesema imejipanga kuanza ujenzi wa viwanda vidogo 7 vya kutengeneza hewa tiba ya oksijeni ili kupambana na janga la Corona

Hayo yamesemwa na Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu wizara ya fedha na mipango wa Tanzania katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni siku chache baada ya bodi ya Utendaji ya Shirika la fedha la Kimataifa - IMF kutangaza kutoa mkopo wa dharura wa dola Milioni 567.25 kwa Tanzania ili iweze kukabiliana na janga la COVID-19.

“Kulingana na andika tulilowasilisha IMF, kwenye eneo la afya, tutatengeneza viwanda vidogo vya kutengeneza hewa tiba ya oksijeni, ambapo kuna viwanda kama 7 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa oksijeni. Kuna viwanda vingine vilishaanza kutengenezwa kwa fedha za serikali baada ya serikali kutoa bilioni 10 kwa ajili ya kununua mitungi na kutengeneza viwanda vidogo vya kutengeneza oksijeni. Kwahiyo kwa fedha hizi tutaweza kutengeneza viwanda kwenye hospitali nyingine za mikoa saba.”

Tutuba ameongeza kuwa kwenye eneo hilo la afya pia wanatarajia kununua mavazi maalum kwa wahudumu wa afya PPEs na baadhi ya fedha zitaelekezwa kwenye ajira za wahudumu wa afya kwakuwa wao ndio wapo mstari wa mbele kupambana na COVID-19. 

Pamoja na kujipanga kutoa elimu zaidi kwa umma ya kujilinda wasipate maambukizi ya janga hilo linaloitesa dunia kwa miezi zaidi ya 18 sasa, Katibu Mkuu huyo wa Fedha wa Tanzania amesema wataenda mbali zaidi kwenye sekta ya elimu. 

“Suala la COVID-19 linataka watu wasikae kwenye msongamano mkubwa, sasa bado tunachangamoto, mashuleni watoto wamerundikana kwahiyo fedha hizi zitatuwezesha kujenga baadhi ya madarasa na madawati ili badala wanafunzi kukaa watatu katika dawati moja, ikiwezekana wakae hata wawili hasa katika maeneo yenye misongamano mikubwa.”

Amegusia pia kuweka mazingira bora kwa wasichana “kutakuwa na fungu kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa mabweni kwenye maeneo ambayo shule hasa za wasichana ambazo zimebanana sana”  

Hifadhi zinachukua hatua kukabiliana na COVID-19 na kuhakikisha utalii salama.Simba katika hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya
UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch
Hifadhi zinachukua hatua kukabiliana na COVID-19 na kuhakikisha utalii salama.Simba katika hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya

Sekta ya Utalii

Tutuba amesema sekta ya utalii ambayo inaliingizia taifa hilo fedha nyingi imeathirika kwa kiasi kikubwa mpaka kufikia nchi hiyo kuanza kulipa mishahara ya wafanyakazi wa hifadhi zake za Taifa, TANAPA pamoja na Mamlaka ya hifadhi ya Ng’orong’oro. Kwa fedha walizopata kutoka IMF wataendelea na ulipaji wa mishahara pamoja na ukarabati wa miundombinu. 

Kuhusu kuwasaidia wafanyabiashara wa utalii binafsi ambao nao wameathirika kwakukosa watalii sababu yajanga la CORONA. Tutuba amesema “tutaangalia namna ya kuwawezesha kwa kuweka miundombinu na mifumo rasmi itakayo wawezesha, kama kutakuwepo na mkopo mdogo kwa ajili ya atakayekuwa amekwama.” 

Tutuba amesema serikali ya Tanzania imejidhatiti kuhakikisha yale yote waliyoahidi kwenye andiko lililowawezesha kupata fedha wanayatimiza kwakuwa wametumia muda mrefu kujadiliana na kufikia makubaliano ya matumizi ya fedha hizo ambazo pia zitanufaisha wananchi wa kaya masikini moja kwa moja kupitia mfuko wa kusaidia kaya masikini TASAF.