Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda unatutupa mkono kuepuka janga la mabadiliko ya tabianchi:UN Ripoti 

Watu wakiwa katika mto uliofurika Magharibi mwa Haiti baada ya daraja kusombwa na maji kufuatia kimbunga Matthew
MINUSTAH/Logan Abassi
Watu wakiwa katika mto uliofurika Magharibi mwa Haiti baada ya daraja kusombwa na maji kufuatia kimbunga Matthew

Muda unatutupa mkono kuepuka janga la mabadiliko ya tabianchi:UN Ripoti 

Tabianchi na mazingira

Kupunguzwa kwa muda kwa uzalishaji wa hewa ukaa kulikosababishwa na masharti ya kimataifa ya watu kusalia majumbani wakati wa janga la corona au COVID-19 hakukupunguza kasi ya kuendelea kwa mabadiliko ya tabianchi. Viwango vya gesi chafuzi vimevunja rekodi, na dunia iko njiani  kuelekea hatari joto kali la kupindukia,  imeonya ripoti ya mabadiliko ya tabia nchi iliyotolewa leo na mashirika  mbalimbali. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kihistoria “Muungano katika sayansi 2021”, "hakuna ishara ya kurejea katika hali bora ya mazingira ", kwani uzalishaji wa hewa ukaa unaongezeka kwa kasi baada ya kupungua kwa muda mfupi muda mwaka 2020 kwa sababu ya COVID-19, na hatukaribii hata chembe kutimiza malengo yaliyowekwa na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. 

Akiweka sauti yake katika ripoti hiyo kupitia ujumbe maalum wa video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza kwamba "Tumefikia kilele cha kuhitaji hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Usumbufu wa mabadiliko ya tabianchi kwa hali ya hewa yetu na dunia yetu tayari ni mbaya kuliko vile tulivyofikiria, na unakwenda kwa kasi zaidi kuliko ilivyotabiriwa, na ripoti hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyo kwenda kombo na lengo letu”. 

Dunia iko hatarini 

Kulingana na wanasayansi, kuongezeka kwa joto duniani tayari kunachochea matukio mabaya ya hali ya hewa ulimwenguni, na athari zinazoongezeka kwa uchumi na jamii. Kwa mfano, mabilioni ya masaa ya kazi yamepotea kwa sababu ya joto kali. 

“Sasa tuna mara tano zaidi ya idadi ya majanga ya hali ya hewa yaliyorekodiwa kuliko ilivyokuwa mwaka wa 1970 na ni ya gharama kubwa mara saba. Hata nchi zilizoendelea zaidi zimekuwa hatarini”, amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Bwana Guterres alinukuu jinsi Kimbunga Ida kilivyowaacha gizani bila umeme  hivi karibuni zaidi ya watu milioni moja huko New Orleans, na mjini wa New York ulivyoghubikwa na mvua kubwa iliyovunja rekodi ambayo iliua watu wasiopungua 50 katika jimbo hilo. 

Guterres ameonya kwamba "Matukio haya hayangewezekana bila mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu. Moto wa gharama kubwa, mafuriko na matukio ya hali mbaya ya hali ya hewa vinaongezeka kila mahali. Mabadiliko haya ni mwanzo tu wa hali mbaya inayokuja.” 

Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika
Unsplash/Mikhail Serdyukov
Mabadiliko ya tabianchi yameongeza hatari ya hali ya hewa kavu, ya joto ambao inachangia kuchochea moto wa nyika

Mustakbali mbaya 

Ripoti hiyo inaunga mkono takwimu na maonyo yaliyotolewa kutoka kwa wataalam mwaka jana ambapo walisema wastani wa joto ulimwenguni kwa miaka mitano iliyopita umekuwa katika kiwango cha juu kabisa, na kuna uwezekano mkubwa kuwa joto litavunja rekodi na kuwa juu ya nyuzi toto 1.5 ° Celsius juu ya zama za kabla ya maendeleo ya viwanda, katika miaka mitano ijayo. 

Taswira iliyochorwa na Umoja wa sayansi ni mbaya, hata kwa hatua kubwa ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, viwango vya bahari vitaendelea kuongezeka na kutishia visiwa vidogo na idadi ya watu wa pwani duniani. 

Katibu Mkuu amehimiza kwamba “Kwa kweli tumepitwa na wakati. Lazima tuchukue hatua sasa ili kuzuia uharibifu zaidi usioweza kurekebishwa. COP26 itakayofanyika Novemba hii lazima iwe alama ya hatua hiyo ya kugeuza mwelekeo. Kufikia wakati huo tunahitaji nchi zote kujitolea kufanikisha kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo  katikati ya karne hii na kutoa mikakati ya wazi na ya kuaminika ya muda mrefu kufika ya kufikia lengo hilo.” 

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2021, unaojulikana pia kama COP26, umepangwa kufanyika katika mji wa Glasgow, Scotland kati ya tarehe 31 Oktoba na 12 Novemba 2021.  

Mkutano huo muhimu unatarajiwa kuweka hatua dhidi ya mabnadiliko ya tabianchi kwa muongo ujao.

Kimbunga Amphan kilikumba jimbo la mpakani mwa India na Bangladesh Mei 2020 na kusababisha uharibifu mkubwa
UNU-EHS/Tanmay Chakraborty
Kimbunga Amphan kilikumba jimbo la mpakani mwa India na Bangladesh Mei 2020 na kusababisha uharibifu mkubwa

"Lazima tupate haraka mafanikio ya kukabiliana na hali na uthabiti, ili jamii zilizo katika mazingira magumu ziweze kudhibiti hatari hizi zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi. Natarajia masuala haya yote yatatuliwe katika COP26. Mustakabali wetu uko hatarini ”, Bwana Guterres amesisitiza. 

Naye Profesa Petteri Taalas, katibu mkuu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani ameongeza kuwa "Bado hatuko kwenye njia sahihi ya lengo la  Paris la kusalia na nyuzi joto 1.5 hadi 2 digrii, ingawa mambo mazuri yameanza kutokea na nia ya kisiasa ya kupunguza mabadiliko ya tabianchi inakua wazi zaidi lakini kufanikiwa katika juhudi hizi, lazima tuanze kuchukua hatua sasa. Hatuwezi kusubiri kwa miongo kadhaa kuchukua hatua, lazima tuanze kuchukua hatua  katika muongo huu ”. 

Ripoti hiyo pia inataja hitimisho la ripoti ya hivi karibuni ya IPCC kuwa kiwango cha mabadiliko ya hivi karibuni katika mfumo wa hali ya hewa haujawahi kutokea kwa karne nyingi hadi maelfu ya miaka, na ni wazi kuwa ushawishi wa wanadamu umeongeza joto angani, baharini na ardhini.