Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya ahadi, Burundi yaendelea kukiuka haki za binadamu na kufunga malngo wa demokrasia: HRC

Watoto wakiteka maji machafu katika mto karibu na nyumbani jimbo la Ruyigi nchini Burundi. Septemba 14, 2017
© UNICEF/UN0185046/Haro
Watoto wakiteka maji machafu katika mto karibu na nyumbani jimbo la Ruyigi nchini Burundi. Septemba 14, 2017

Licha ya ahadi, Burundi yaendelea kukiuka haki za binadamu na kufunga malngo wa demokrasia: HRC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Burundi imesema licha ya ahadi za awali za Rais Évariste Ndayishimiye za kuboresha haki za binadamu nchini mwake na kurejesha utawala wa sheria, bado hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kutimiza ahadi hizo, huku jukwaa la kidemokrasia likiendelea kufungwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ukitamalaki tangu Rais huyo achukue madaraka Juni 2020.

Akiwasilisha ripoti yao ya tano ya uchunguzi kwenye Baraza la haki za binadamu mjini Geneva Uswis hii leo mwenyekiti wa tume hiyo Doudou Diène amesema "Hata kama nchi inaonekana kuwa katika mstari wa kuelekea kawenye maisha ya kawaida , bado kuna sababu za kutosha za kusalia na wasiwasi mkubwa juu ya hali mbaya ya haki za binadamu nchini Burundi. Tunatoa wito kwa kila mtu anayehusika na Burundi kuiangalia kwa kina zaidi. Tangu kuapishwa kwa Rais Ndayishimiye miezi 15 iliyopita, sio tu kwamba ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea kutokea, lakini pia katika masuala mengine hali imekuwa mbaya zaidi". 

Akitoa mfano amesema, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu umetokea katika muktadha wa mashambulizi mengi ya silaha yaliyofanywa tangu Agosti 2020. “Wakati wa kutafuta watu wanaodaiwa kuhusika katika mashambulizi ya silaha au kushirikiana na vikundi vya waasi, vikosi vya usalama viliwalenga sana wanachama kutoka chama kikuu cha upinzani cha (CNL), wanachama wa zamani wa Jeshi la linalotawaliwa na Watutsi wengi (ex-FAB), waliorejea na baadhi ya wanafamilia wao. wengine waliuawa, na wengine walitoweka au waliteswa wakati wakizuiliwa kiholela." 

Ingawa kiwango cha vurugu za kisiasa kilipungua mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, hali ya kisiasa inabaki kuwa ya kutovumilia wapinzani.  

Wanachama wa vyama vya upinzani, haswa CNL, bado wanalengwa mara kwa mara na vizuizi vya unyanyasaji na wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama vile kutoweka, kukamatwa kiholela, kuwekwa kizuizini na kuteswa, haswa tangu Juni 2021. 

Katika ripoti hii mpya, tume inabainisha ishara zinazopingana zinazotolewa na mamlaka kwani wakati ikiondoa vikwazo kadhaa vilivyowekwa kwa asasi za kiraia na vyombo vya habari na kuwaachilia watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari, kwa upande mwingine serikali ilichukua hatua sanjari kukaza udhibiti wake katika kazi za mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali NGOs na mara kwa mara kujenga uadui dhidi ya uandishi wa habari huru. 

Ripoti imewataja wakiukaji wakubwa wa haki na unyanyasaji huo kuwa ni pamoja na shirika la kijasusi la kitaifa SNR, maafisa wa polisi na jumuiya ya vijana wa chama tawala cha CNDD-FDD wajulikanao kama Imbonerakure. 

Ripoti imesisitiza kuwa “wahusika hao wanaojulikana kwa ukatili wao wameendelea kufurahia ukwepaji wa sheria kwa makosa ambayo mengine yanaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.” 

Kwa upande wake Françoise Hampson, mjumbe wa tume hiyo ameainisha kuwa “Utawala wa sheria umeendelea kudidimia nchini Burundi licha ya ahadi za awali za Rais Ndayishimiye za kuurejesha. Nchini Burundi mahakama haiwezi kuaminiwa kudhibiti au kurekebisha haki za binadamu. Ripoti yetu inaonyesha jinsi gani utawala unavyojiimarisha katika kudhibiti mahakama katika uongozi mpya. 

Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu haki za binadamu Burundi ndio chombo pekee cha kimataifa kilichosalia katika kipindi cha miaka mitano sasa kikiorodhesha na kuripoti kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Burundi.