Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpaka sasa saa trilioni 1.8 zimepotea za watoto kushindwa kuhudhuria madarasani:UNICEF

Ufunguaji washule umechelewa kutokana na janga la COVID-19 na kuathiri takriban watoto milioni 140
© UNICEF/Daniele Volpe
Ufunguaji washule umechelewa kutokana na janga la COVID-19 na kuathiri takriban watoto milioni 140

Mpaka sasa saa trilioni 1.8 zimepotea za watoto kushindwa kuhudhuria madarasani:UNICEF

Utamaduni na Elimu

Umoja wa Mataifa umetengeneza darasa maalum katika Makao Makuu yake yaliyoko jijini New York Marekani na kuweka madawati na saa inayoonesha muda ambao wanafunzi wameshindwa kuingia darasani kutokana na janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19.

Ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa leo hii kunafanyika tukio la aina yake. 
 
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limetengeneza darasa la mfano lenye madawati 18 nje ya lango kuu la kuingilia wajumbe wa mjadala mkuu wa  #UNGA76.


Madawati 18 na mabegi ya wanafunzi yakiwa yamewekwa nyuma ya viti yakiashiria miezi 18 tangu janga la janga la Corona lilipoikumba dunia na kusababisha shule pamoja na maeneo mengine kufungwa. 
 
Na takwimu zinaonesha kuwa mpaka sasa zaidi ya saa Trililioni 1.8 za wanafunzi kukaa darasani kusoma zimepotea na bado zinaendelea na ndio maana imeweka saa inayoonesha muda unavyozidi kuyoyoma.
 
Akizindua darasa hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “ Wiki ijayo ( Tarehe 20 Septemba 2021) tutafungua milango  kuwakaribisha wajumbe kutoka kote ulimwenguni. Lakini katika nchi nyingi, milango ya shule itabaki imefungwa kwa watoto na vijana. Ni lazima tutoe kipaumbele katika kufungua shule na kuwasaidia wale waliopoteza masomo  wakati wa janga hilo. Hakuna muda wa kupoteza.”

Eneo hilo maalum la mfano wa darasa litaendelea kuwepo kuanzia leo tarehe 17 Septemba hadi tarehe 27 Septemba ambapo itakuwa ndio mwisho wa mjadala Mkuu wa  Wazi wa UNGA76 .
 
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema "Kila saa ambayo mtoto hutumia darasani ni ya thamani na inatoa fursa ya kupanua upeo wake na kuongeza uwezo wake. Na muda unavyopotea, idadi kubwa ya fursa hupotea.  Mpaka sasa saa trilioni 1.8 zimepotea na bado zinaendelea kupotea, muda huu usioweza kueleweka,nwakati usioweza kueleweka. Usawa isioeleweka unaweka vipaumbele katika kupunguza athari za janga la COVID-19 lakini hauweki maisha ya baadaye ya watoto wetu mbele.  Tunaweza, na lazima tufungue shule haraka iwezekanavyo. Muda unaendelea kuyoyoma.”

UNICEF imetoa wito kwa wakuu wa nchi, mikoa na wilaya kufungua shule na kusimamia masharti yote ya kujikinga na Corona ikiwemo uvaaji wa barakoa, uwepo wa maji ya kunawa na vitakasa mikono pamoja na kuhakikisha madarasa yanapitisha hewa ya kutosha.