Ukiwaengua raia, demokrasia katu haiwezi kuishi wala kusharimi- Guterres

15 Septemba 2021

Leo ni siku ya kimataifa ya demokrasia ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi zote duniani kuimarisha uthibiti wa kidemokrasia, na wananchi wote duniani kuweka ahadi ya kutambua na kulinda haki za binadamu pamoja na kuheshimu utawala wa sheria kama msingi wa demokrasia.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani, Guterres imeeleza viongozi wa nchi wanatakiwa kukuza mazoea ya utawala bora hususan katika kipindi cha mizozo iwe ya afya, mazingira au kifedha. 

Amezishauri nchi kushughulikia changamoto za ulimwengu kama usawa wa kijinsia, mifumo duni ya afya, elimu, upatikanaji wa mtandano wa internet na huduma nyingine za kimtandao. Amesema ukosefu wa usawa ambao uko kihistoria pia ni tishio la kidemokrasia.

Ujumbe huo wa Guterres umesisitiza kuwa iwapo nchi zinataka kuimarisha demokrasia inamaanisha zinatakiwa kukubali ushirikishwaji wa dhati wakati wa kufanya maamuzi pamoja na maandamano ya amani. 

Ameongeza kuwa jamii inatakiwa kupewa fursa ya kupaza sauti ambazo kijamii zinakuwa zimetengwa. Kunyamazisha sauti za wanawake, dini, makabila madogo, jamii za asili, watu wenye ulemavu, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari ni kizuizi cha kuunda jamii zenye afya na kwamba demokrasia haiwezi kuishi, achilia mbali kushamiri bila kuwapa nafasi raia. 

Vijana raia wa Msumbiji wakionesha vidole vyenye wino wa buluu wakiashiria wameshapiga kura kwenye uchaguzi
UNDP/Rochan Kadariya
Vijana raia wa Msumbiji wakionesha vidole vyenye wino wa buluu wakiashiria wameshapiga kura kwenye uchaguzi

 Sheria za dharura

Akihitimisha ujumbe wake wa siku hii Guterres amesema ili kulinda demokrasia inamaanisha pia kuondoa sheria za dharura iwapo majanga yaliyosababisha kuwekwa yamepungua, akieleza kuna baadhi ya mataifa na tasisi za sekta za usalama wanategemea nguvu ya sheria za dharura kama njia za mkato kwenye kufanya maamuzi yao. 

Amesema kwa kutumia sheria hizo, mamlaka zinaweza kuingiza mifumo ya kisheria na kuwa ya kudumu na vitendo hivyo vinadhoofisha utawala wa sheria na haki za binadamu ambao ndio msingi wa demokrasia.    

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter