Skip to main content

Watu 81,000 hadi 137,000 hufa kila mwaka kwa kung'atwa na nyoka:WHO

WHO  hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo  pichani.
Thea Litschka-Koen
WHO hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo pichani.

Watu 81,000 hadi 137,000 hufa kila mwaka kwa kung'atwa na nyoka:WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limezindua jukwaa maalum mtandaoni kwa lengo la kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu hatari ya kung'atwa na nyoka wenye sumu na wapi waliko nyoka hao hatari zaidi duniani.

Shirika hilo linasema watu 81,000 hadi 137,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari zinazosababishwa na kung'atwa na nyoka wenye sumu.

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo na WHO wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo mjini Geneva Uswisi, ingawa idadi kamili ya waliong'atwa na nyoka hadi sasa haijulikani lakini makadirio yanaonyesha kwamba takriban watu milioni 5.4 hung'atwa na nyoka kila mwaka huku milioni 2.7 kati yao na nyoka wenye sumu kali ambao husababisha athari mbaya kwa mamilioni ya maisha ya watu na wengi wao wakiwa masikini. 

Mbali ya vifo vya watu hadi 137,000 kila mwaka, kung'atwa na nyoka pia kumewaacha mamilioni ya watu na vilema vya maisha. 

WHO inasema kung'atwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa ambayo inapelekea ulemavu wa maisha na kukatwa viungo. 

Shirika hilo limeongeza kuwa kung'atwa na nyoka ni moja ya magonjwa yaliyopuuzwa NTDs  ambayo athari zake ni kubwa na mbaya kuliko inavyodhaniwa.  

Waathirika wakubwa ni watu wanaofanyakazi katika sekta ya kilimo na watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hasa vijijini.

Mathalani barani Asia watu wapatao milioni 2 hudhurika na sumu ya nyoka kila mwaka wakati Afrika watu 435,000 hadi 580,000 huhitaji matibabu kila mwaka baada ya kung'atwa na nyoka. 

Kwa mujibu wa WHO ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kung'atwa na nyoka mosi ni lazima kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, pili kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, tatu kuimarisha mifumo ya afya na nne kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hii.