Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndege zaanza kuingiza misaada Afghanistan

Ndege ya shirika la Anga la Umoja wa Mataifa UNHAS ikiondoka Islamabad nchini Pakistan ikiwa ni safari yake ya kwanza kwenda Kabula tangu Taliban washike madaraka
UNHAS
Ndege ya shirika la Anga la Umoja wa Mataifa UNHAS ikiondoka Islamabad nchini Pakistan ikiwa ni safari yake ya kwanza kwenda Kabula tangu Taliban washike madaraka

Ndege zaanza kuingiza misaada Afghanistan

Msaada wa Kibinadamu

Ndege za shirika la Anga la Umoja wa Mataifa zinazosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP zimeanza tena safari zake za kupeleka msaada Kabul nchini Afghanistan na kuwawezesha wafanyakazi wa kibinadamu kuwafikia wananchi wenye uhitaji.

Nchini Afghanistan zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wanahaha kupata mlo wa familia, Ghulam Dastagir mwenye umri wa miaka 58, baba wa familia ya watu 10 anasema maisha ni magumu mno. 
 
“Hali ni mbayá, tunataabika, hivi sasa hatuna chochote, bei ya bidhaa nayo inapanda kila siku, watu hawana pesa wala kazi, hakuna kazi. Mafuta ya lita 10 ni Afghani 1400 sawa na dola 16. Ikiwa mtu huwezi kupata dola 4 kwa mwezi, tutapata wapi fedha hizo hata za kununulia mafuta? “ 
 
Mashirika ya kibinadamu nayo yanahangaika kila uchao kupata msaada wa kibinadamu kwa kuwa wao ni mashuhuda wa hali ngumu inayokabili wananchi, kama anavyoeleza Mkurugenzi wa WFP nchini Afghanistan Mary-Ellen McGroarty. 
 
“Watu watatu kati ya wanne tayari wanakopa chakula. Vyakula wanavyokula havina virutubisho, kwa hiyo kimsingi, wameachana kabisa na kula nyama, maziwa na mboga za majani. Pia wanapunguza milo ya siku. Mara nyingi  wazazi wanaamua kutokula ili wawaachie Watoto wale. Kimsingi kila mtu anakabiliana na njaa kali.” 
 
Baada ya uongozi mpya wa Taliban kushika madaraka anga ya Afghanistan ilifungwa, lakini mwanzoni mwa wiki hii, ndege za WFP zimeruhusiwa kuingiza misaada kama chakula na vifaa vya matibabu. 
 
Bi. McGroarty anasema wameweka ofisi za kugawa misaada maeneo 6 ili kuhakikisha usambazaji wa haaraka wa msaada huku akiendelea kuwaomba wahisani kuwasaidia zaidi. 
 
“Mipango ya WFP kwa sasa ni kuhakikisha tunaingiza chakula kingi nchini kadri iwezekanavyo kabla ya kuanza kwa majira ya baridi, maana theluji ikishaanza tu inakuwa ngumu kufikia jamii ziishizo milimani kwa sababu  mawasiliano hukatika. Tumeomba kwa wahisani dola milioni 200. Tunahitaji fedha hizo sasa ili tuweze kununua chakula na kukiingiza nchini kwa wakati.” 
 Mpaka sasa WFP imewafikishia msaada wa chakula watu milioni 6.4 nchini Afghanistan huku lengo likiwa kufikia watu milioni 14 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2021.