Tambueni chanjo zote za COVID-19 zilizoidhinishwa na WHO

14 Septemba 2021

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaka nchi zote duniani kutambua chanjo zilizoidhinishwa na shirika hilo kwa matumizi ya dharura dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 wakati huu ambapo bado kuna pengo kubwa la utoaji wa chanjo hiyo katika maeneo mbalimbali duniani hususan barani Afrika.
 

Dkt. Tedros amesema hayo  hii leo mjini Geneva, Uswisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uwiano wa mgao na utoaji wa chanjo dhidi ya Corona duniani kote.
Tamko hilo la WHO limekuja wakati baadhi ya nchi hazitambui chanjo zingine ambazo zimeidhinishwa na shirika hilo ili kukinga binadamu dhidi ya Corona.

Chanjo zilizoidhinishwa ni pamoja na Pfizer/BioNTech, Astrazeneca- ya Korea Kusini au SK Bio, Astrazeneca ya kutoka taasisi ya Serum nchini India, Janssen, Moderna, Sinopharm na .Sinovac.

Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.
UNICEF/Daniel Msirikale
Chanzo zilizotolewa kwa Tanzania kwa msaada wa Marekani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaka chanjo za Corona au COVID-19, COVAX, na ziliwasili tarehe 24 Julai 2021.

Kwa kuzingatia kuwa hadi sasa ni asilimia 2 tu ya chanjo zote bilioni 5.7 dhidi ya Corona ndio zimekwenda Afrika pekee, Dkt. Tedros ametaka  kampuni zinazotengeneza chanjo kupatia  kipaumbele upelekaji wa chanjo kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kusambaza chanjo ya Corona, COVAX na ule wa Muungano wa Afrika, AVAT ili zipelekwe kule ambako bado kuna pengo.

Halikadhalika amesihi nchi ambazo tayari angalau zimefikia kiwango kizuri cha utoaji chanjo zitimize ahadi zao za kupeleka chanjo dhidi ya Corona kule kwenye uhitaji zaidi sambamba na kupeleka teknolojia rahisi ya utengenezaji wa chanjo kwenye maeneo ambako kumeanzishwa viwanda vya kutengeneza chanjo za Corona.

Dkt. Tedros amesema ataendelea kusisitiza suala la uwiano wa mgao wa chnajo duniani na kwamba, “sitojali iwapo nitaonekana narudiarudia hoja hii hadi pale ambapo tutafikia uwiano wa chanjo.”

Amesisitiza kuwa kadri ukosefu wa usawa katika mgao wa chanjo utakavyoendelea, vivyo hivyo virusi vya corona vitaendelea kusambaa na kubadilika, vivyo hivyo maisha ya kijamii na kiuchumi yataendelea kuvurugika na kutakuwa na fursa kubwa zaidi ya minyumbuliko ya virusi vya Corona kuibuka na chanjo kushindwa kuwa na ufanisi.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter