Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo bora ya chakula ni lulu kwa maisha na mazingira:Guterres

Mkulima nchini Gambia akionesha mpunga aliopanda lakini umeshindwa kuota kutokana na uhaba wa maji
© FAO/Seyllou Diallo
Mkulima nchini Gambia akionesha mpunga aliopanda lakini umeshindwa kuota kutokana na uhaba wa maji

Mifumo bora ya chakula ni lulu kwa maisha na mazingira:Guterres

Masuala ya UM

Kuelekea mkutano wa ngazi ya juu wa mifumo ya chakula unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 Septemba mwaka huu 2021 wakati wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema mifumo ya chakula ndio nguzo ya Maisha na mazingira. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini New York Marekani Bwana Guterres amesema “Jumuiya ya kimataifa ina nafasi muhimu ya kusaidia kuendeleza maono ya ajenda ya 2030 kwa kubadilisha jinsi tunavyozalisha, kusindika na kula vyakula.” 

Ameongeza kuwa “mifumo mizuri ya chakula inaweza kusaidia kuzuia mizozo, kulinda mazingira na kutoa afya na maisha bora kwa wote.” 

 Penye chakula, kuna matumaini. 

Taarifa yake imeendelea kusema kuwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, wakati janga la corona au COVID-19 lilipotutenganisha, Mkutano wa mifumo ya chakula uliwaleta watu pamoja kupitia mchakato mzuri wa ushiriki wa kimataifa. 

Waliungana kwa wazo rahisi kwamba “Chakula kinaweza kutusaidia kuharakisha vitendo na kuleta suluhisho za kutimiza malengo yote ya maendeleo endelevu SDGs na na kujikwamua vyema kutoka kwa COVID-19.” 

Amesisitiza kwamba wakati viongozi wanajiandaa kwa mkutano wa kihistoria wa mifumo ya chakula hapo tarehe 23 Septemba kwenye Baraza Kuu, “nawasihi kila mtu aje na ahadi kubwa za kulisha matumaini ya maisha bora ya baadaye. Ni jukumu letu la kimaadili kutimiza ahadi zetu za kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.”