Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipochukua hatua watoto milioni 1 wataangamia kwa unyafuzi Afghanistan:UNICEF

Mtoto akiwa katika hospitali ya watoto ya Gandhi mjini Kabul nchini Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Mtoto akiwa katika hospitali ya watoto ya Gandhi mjini Kabul nchini Afghanistan

Tusipochukua hatua watoto milioni 1 wataangamia kwa unyafuzi Afghanistan:UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

•     Watoto milioni 1 wako hatarini kwa utapiamlo
•    Zaidi ya milioni 9.5 wameacha shule wengi ni wasicha
•    Msaada unahitajika kunusuru afya yao na elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeonya kwamba karibu watoto milioni moja nchini Afghanistan wanakabiliwa na tishio kubwa la kupata unyafuzi kutokana na ukame na vita vinavyoendelea.

Katika hospitali ya watoto ya Indra Gandhi mjini Kabul hali ya utapiamlo uliokithiri au unyafuzi ni dhahiri  wakati timu ya UNICEF ikiongozwa na mwakilishi wa shirika hilo mjini Kabul Herve Ludovic na uongozi wa hospitali walipotembelea  wodi ya watoto wenye utapiamlo na inayotoa huduma za wanawake baada ya kujifungua. 

Kwa mujibu wa uongozi wa hospitali hii baada ya mapigano kupungua sasa wanatarajia watoto wengi zaidi wataletwa kupata matibabu ya utapiamlo na maradhi mengine. 

Changamoto kubwa shirika la UNICEF linasema ni mashirika mengi ya misaada kuondoka wiki chache zilizopita baada ya vikosi vya Marekani kufungasha virago na ulinzi waliokuwa wakiutoa mjini Kabul kuota mbawa na hivyo kuacha mamilioni ya watu wakiwemo watoto katika zahma kubwa ikiwemo ya chakula, matibabu, maji, malazi na mahitaji mengine muhimu.

Hata hivyo bado UNICEF ina matumaini ya mustakbali bora wa watoto wa Afghanistan endapo hatua madhubuti zitachukuliwa hasa baada ya shule kufunguliwa tena kwa watoto wa darasa la 1 hadi la sita katika shule nyingi kufuatia amri  ya serikali hapo Agosti 24.

 

Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu
© UNICEF/Marko Kokic
Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu

Moja ya shule zilizofunguliwa ni shule ya wavulana ya Sultan Ghaiathudin Ghori yenye wanafunzi takriban 6,500 wa darasa la 1 hadi la 12 . Wanafunzi hawa wanafurahia tena utoto wao na haki ya kupata elimu, japo katika majimbo mengine shule zimefunguliwa kwa watoto wa darasa la 1 hadi 6 pekee na kuanzia darasa la 7 na kuendelea haijulikani lini watarejea shuleni. 

UNICEF inasema nchini Afghanistan hata kabla ya kuzorota kwa usalama hali ya kibinadamu ilikuwa mbaya na watoto zaidi ya milioni 4.2 , asilimi 60 wakiwa ni wasichana walikuwa wameacha shule , na na sasa idadi imengezeka zaidi kutokana na COVID-19 na vita.
leo hii takwimu zinaontesha watoto milioni 9.5 ambao huwa katika shule rasmi hawako shuleni na asilimia 38 kwati yao ni wasichana huku  wengine 500,000 ambao huwa katika mfumo usio rasmi wa masomo nao pia wameacha shule. 

UNICEF imetoa wito wa hatua kuchukuliwa haraka kunusuru mamilioni ya watoto wa taifa hilo sio tu kwa utapiamlo na usalama bali pia kwa mustakbali wao wa elimu.