Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yakumbushwa ahadi ya uwepo wa asilimia 30 ya wanawake wabunge

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ( Aliyevaa kilemba cha blu bahari) amekutana na viongozi wanawake mjini Mogadishu, Somalia
UNSOM
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ( Aliyevaa kilemba cha blu bahari) amekutana na viongozi wanawake mjini Mogadishu, Somalia

Somalia yakumbushwa ahadi ya uwepo wa asilimia 30 ya wanawake wabunge

Wanawake

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, amehitimisha ziara yake ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika kwa kutembelea nchi ya Somalia na kuelezea mshikamano wake na wito kwa wanawake wa Somalia kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu. 

Katika mikutano yake mjini Mogadishu, Bi Mohammed amezungumzia uchaguzi wa wabunge kuwa ni fursa muhimu ya kujenga maendeleo yaliyopatikana katika ushiriki wa kisiasa wa wanawake.  

"Somalia imefikia hatua muhimu katika uchaguzi wake uliopita mwaka 2016/17 kwa kufikia asilimia 24 ya viti vya bunge vilijazwa na wanawake, na nina matumaini kuwa nchi itaendeleza hili kwa kuongeza wanawake zaidi kushiriki.” Amesema Bi Mohammed na kusisitiza kuwa “Ikiwa nchi itahakikisha kiwango cha asilimia 30 kinatimizwa, itakuwa ni hatua muhimu ya kwanza kwenda kwenye uwakilishi kamili na jamii inayojumuisha watu wote. Amani kamili haitatokea bila wanawake”.

Hivi sasa, Somalia inafanya uchaguzi wa mawaziri, na inajiandaa kwa uchaguzi wa wabunge, linalojulikana kama Bunge la watu. 
Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kimataifa nchini Somalia wamekuwa wakijishughulisha katika kusaidia juhudi za kitaifa za kuendeleza uchaguzi huo, huku wakionesha kuungwa wanawake kushiriki kwenye siasa

Akiwa mjini Mogadishu, Naibu Katibu Mkuu huyo amekutana na Rais wan chi hiyo Mohamed Abdullahi Mohamed 'Farmaajo,' pamoja na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble pamoja na Baraza la ushauri la Kitaifa -NCC ambalo wanachama wake wanajukumu la kutoa mwelekeo kamili wa uchaguzi.

“Waziri Mkuu Roble na wanachama wengine wa NCC wameonesha uongozi mzuri na kujitolea kuendeleza ushiriki wa kisiasa wa wanawake, pamoja na kupitia hatua maalum kama vile kupunguza ada kwa wagombea wanawake na kuteua mabalozi wa hiari wenye jukumu la kutetea na kushawishi ushirikishwaji zaidi wa wanawake” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Amewashauri pia kuwa itakuwa muhimu kama watakubaliana juu ya utaratibu maalum wa jinsi ahadi ya uwakilishi wa wanawake asilimia 30 utafikiwa katika uchaguzi ujao.

Kabla ya kwenda Somalia Naibu katibu Mkuu huyo alitembelea pia Kenya na Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na kufanya mazungumzo na marais wa nchi hizo.