Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji wa haki za binadamu umefurutu ada Tigray: Bachelet

Mzozo kaskazini mwa Ethiopia imesababisha mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi
© UNICEF/Christine Nesbitt
Mzozo kaskazini mwa Ethiopia imesababisha mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi

Ukiukwaji wa haki za binadamu umefurutu ada Tigray: Bachelet

Msaada wa Kibinadamu

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema ukiukwaji wa haki za binadamu jimboni Tigray nchini Ethiopia umefurutu ada na sasa mapigano yanayoendelea yamesambaa katika majimbo ya Jirani ya Afar na Amhara na kutishia kusambaa katika eneo lote la pembe ya Afrika. 

Akizungumza katika kikao cha 48 cha Baraza la Haki za Binadamu kuhusu hali ya Tigray kinachoendelea mjini Geneva Uswis, Michelle Bachelet amesema “katika miezi michache iliyopita, watu wengi wamewekwa kizuizini, kumekuwa na mauaji, uporaji wa kimfumo, na unyanyasaji wa kijinsia masuala yalnayoendelea kuunda mazingira ya hofu na kusambaratisha hali ya maisha ambayo imewalazimisha raia wengi kulihama jimbo la Tigray. Mateso kwa raia yametamalaki, na adhabu zimeenea.” 

Ameongeza kuwa hata kwa mabadiliko katika mzozo, bado mara kwa mara kumekuwa na ripoti nyingi na mbaya za madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, sheria za kibinadamu na za wakimbizi na unaotekelezwa na pande zote katika mzozo. 


 Asante serikali ya Ethiopia kwa ushirikiano 

Bi. Bachelet ameishukuru serikali ya Ethiopia kwa ushirikiano inaoutoa kupitia kamisheni yake ya haki za binadamu katika kufanya uchunguzi wa pamoja na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Ethiopia kuhusu madai hayo na amesema ruipoti ya pamoja kufuatia uchunguzi wao inatarajiwa kutolewa tarehe 1 Novemba 2021. 

“Ni bayana kuwa visa vilivyoorodheshwa vinajumuisha madai kadhaa ya ukiukaji wa haki za binadamu, pamoja na mashambulio kwa raia, mauaji ya kiholela, mateso, na watu kutoweka miongoni mwa unyanyasaji mkubwa unaoendelea. Ukatili wa kijinsia na kingono umekuwa na tabia ya kuambatana na unyama mkubwa unaojumuisha ubakaji unaofanywa na genge la watu, mateso ya kijinsia na ukatili wa kijinsia unaolengwa kikabila. Ninatambua kujitolea kwa Serikali ili kuhakikisha uwajibikaji kwa unyanyasaji wa kijinsia na ninatarajia kusikia juu ya matokeo ya hatua zozote zilizochukuliwa.” 

Mbali ya kulengwa kwa raia wenye asili ya Tigray, Kamisha huyo mkuu amesema iitisho na mashambulio kwa waandishi wa habari pia vimeripotiwa pamoja na kusimamishwa kwa leseni za vyombo vya habari na vizuizi vya kurusha matangazo na vipindi ikiwa ni pamoja na kuzimwa kwa mtandao na mawasiliano ya simu  za rununu huko Tigray. 

Mtoto akioimwa utapiamlo katika eneo la Adikeh huko Wajirat jimbo la Tigray, Ethiopia
© UNICEF/Christine Nesbitt
Mtoto akioimwa utapiamlo katika eneo la Adikeh huko Wajirat jimbo la Tigray, Ethiopia

  Taswira halisi ya mambo 

Bi. Bachelet ameongeza kuwa tangu kupata udhibiti wa sehemu za Tigray na kupanuka wigo wake hadi mikoa ya jirani, ripoti zimevitambua vikosi vya Tigray kama wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Katika kipindi kinachotathiminiwa na Baraza la haki za binadamu, vikosi vya Tigray vimedaiwa kuhusika na mashambulio dhidi ya raia, pamoja na mauaji ya kiholela yaliyosababisha karibu watu 76,500 kuhama makazi yao huko Afar na inakadiriwa kuwa watu 200,000 wamekimbia huko Amhara. 

Huku watu wengine zaidi ya 200 wakiripotiwa kuuawa katika mapigano ya hivi karibuni kwenye maeneo haya, na watu wapatao 88, wakiwemo watoto, wamejeruhiwa.  

Tarehe 5 Agosti mwaka huu, vikosi vya Tigrayan vilidaiwa kushambulia na kuua watu waliokimbia makazi yao, haswa wanawake, watoto, na wazee, wakiwa wamekaa katika kambi huko Galikoma Kebele, katika Mkoa wa Afar. 
 “Tumepokea pia ripoti nzito za kuajiri watoto kwenye mzozo na vikosi vya Tigray, hatua ambayo ni marufuku chini ya sheria za kimataifa.” Amesisitiza Bi. Bachelet 

Pia ametoa rai kwa pande zote husika katika mzozo wa Tigray kwamba wa “Wahudumu wa haki za binadamu wa kimataifa, kikanda na kitaifa na wahudumu wa masuala ya kibinadamu lazima wapewefursa ya kufikia jimboni Tigray bila vikwazo. “Ninarudia tena wito wangu kwa Serikali ya Eritrea kuhakikisha uwajibikaji wa madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na vikosi vyao katika mkoa wa Tigray.” 

 Suluhu ya mzozo wa Tigray 

Kamishina Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema juhudi zaidi zinahitajika kukomesha vurugu mbaya za kijamii zinazoendfelea zaidi ya jimbo la Tigray. Na suluhu haiwezi kuwa ya kijeshi. 
  
Ninarudia kile nilicholiambia Baraza mwezi Juni mwaka jana kwamba malalamiko lazima yashughulikiwe kwa njia ya mchakato wa amani na juhudi za upatanisho ili kuepusha hatari kwamba Ethiopia itasambaratika, na athari kubwa zaidi kwa nchi hiyo na Pembe ya Afrika. Amesema Bachetet. 

Na kuhitimisha kwamba “Suluhisho la mzozo huko Tigray linaweza kupatikana tu kupitia mchakato wa kisiasa na mazungumzo. Ninapongeza juhudi za upatanishi za Umoja wa Afrika katika suala hili. Natoa wito kwa pande zote kumaliza mara moja uhasama bila masharti yoyote na kujadili kusitisha mapigano.”