Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata walazimu WFP kusitisha mgao wa chakula kwa watu 100,000 Sudan Kusini

Wakazi wa Pibor nchini Sudan Kusini wakisubiri msaada wa chakula.
UNOCHA/Emmi Antinoja
Wakazi wa Pibor nchini Sudan Kusini wakisubiri msaada wa chakula.

Ukata walazimu WFP kusitisha mgao wa chakula kwa watu 100,000 Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limesema litasitisha kwa miezi mitatu mgao wa msaada wa chakula kwa zaidi ya wakimbizi wa ndani 100,000 nchini Sudan Kusini kuanzia mwezi ujao wa Oktoba kutokana na ukata.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, imesema uamuzi huo unalenga kupatia kipaumbele maeneo mengine nchini humo yenye hali mbaya zaidi.

Wakimbizi wa ndani watakaothirika na mkato wa mgao ni wale walioko kwenye kambi huko Wau, Juba na Bor kusini na kwamba sitisho hilo litaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu na wataanza kupata mgao wa chakula kuanzia mwakani ambapo misaada itaanza kutolewa tena kila mwezi kwa wale walioko kambini hadi mwezi Septemba mwaka 2022.

Ingawa hivyo WFP imesema akina mama na watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi miaka 2 na ambao wanaishi kambini wataendelea kupata mgao wa vyakula vyenye virutubisho vya lishe kwa lengo la kukinga na kutibu utapiamlo.

Kipaumbele cha sasa cha mgao wa WFP ni katika kaunti 10 ambazo hufikika kwa tabu, nazo ni zile za Pibor, Akobo, Tonj Kaskazini, Tonj Kusini, Tonj Mashariki, Aweil Kusini, Bor Kusini, Twic Mashariki, Duk na Ayod.

Mwakilishi wa WFP nchini Sudan Kusini Matthew Hollingworth amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema,  hali ngumu zinatahitaji maamuzi magumu, “:tunalazimika kuchukua hatua hizi zenye machungu na kujiongeza na rasilimali kidogo tulizonazo ili kukidhi mahitaji ya wale walio katika hatari ya kukumbwa na njaa kali iwapo hawatopata kabisa chakula.”

Amesema “ingawa michango kutoka kwa wahisani imesaidia WFP kufikia mamilioni ya wahitaji na misaada muhimu ya kuokoa maisha, watu wengi walio hatarini zaidi wanaendelea kukumbwa na machungu ya ukosefu wa uhakika wa chakula na hawawezi kuishi bila msaada endelevu wa chakula.”

Bwana Hollingworth amefafanua kuwa iwapo viwango vya upatikanaji wa fedha kitazidi kupungua, wanaweza wasiwe na uamuzi mwingine zaidi ya kuendeleza kiwango cha makato ya mgao.

WFP imesema itahitaji nyongeza ya dola milioni 154 kwa miezi minne ijayo ili iweze kuendeleza operesheni za mgao wa chakula.

Hatua ya WFP ya kusitisha mgao wa chakula kwa miezi mitatu ni sehemu ya mpango mpana wa shirika hilo uliotangazwa mwezi Aprili mwaka huu katika kambi zote na unaathiri wakimbizi wa ndani na wa kigeni wapatao 700,000 ambao sasa wanapokea nusu ya mgao wa chakula.

Kwa mujibu wa WFP, ukosefu wa uhakika wa chakula nchini Sudan Kusini umeongezeka katika miaka ya karibuni na sasa unaathiri zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wote.

TAGS: Sudan Kusini, WFP, Mgao wa Chakula