Maeneo ya shule sio sehemu za mapigano: Guterres

9 Septemba 2021

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kulinda maeneo ya shule dhidi ya mashambulizi, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekemea tabia ya makundi yanayopigana kuvamia maeneo ya shule, kukamata watu mateka  na vikosi vya ulinzi kufanya maeneo ya shule kama sehemu zao za kuweka kambi za mapigano.

Akizungumza kwenye mkutano wa ngazi za juu ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO pamoja na nchi ya Qatar, Guterres ameanza hotuba yake kwa kuchora taswira ya tukio shuleni akisema, “Fikiria wewe ni mwanafunzi umekaa darasani ukitamani kujifunza, au wewe ni mwalimu umejitolea kubadili kizazi kijacho kwa kuwapa maarifa. Halafu sasa fikiria ghafla unasikia milipuko, na mawazo yote yatakayo kujia baada ya tukio hilo au wakati wowote ukitaka kusoma.”
 
Ameeleza hiyo sio taswira ya kufikirika kwani “Takwimu zilizotolewa kati ya mwaka 2015 na mwaka 2020 na muungano wa Kulinda elimu ulimwenguni, zimeripoti mashambulio ya aina hiyo ya makombora zaidi ya 13,000  yaliyotelekezwa kwenye shule, au vyombo vya kijeshi vya nchi wakitumia maeneo ya shule kurusha makombora wakielekezea wanaopigana nao.”
 
Katibu Mkuu Guterres amesema shule ni sehemu za kutoa na kupokea ujuzi na lazima ziwe sehemu salama kwa kujifunzia kwa amani na usalama kwa kuwa elimu, inabadilisha maisha na kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. 
 

 Azimio la Shule salama 

Akizungumzia Azimio la shule salama, linalo kataza maeneo ya shule kutumika kama maeneo ya vita pamoja na kuainisha hatua zote za serikali zinapaswa kuchukuliwa kulinda shule na maeneo ya kujifunzia.
Guterres amesema, mpaka sasa ni nchi 111 duniani ndio zimepitisha azimio hilo na kutoa wito kwa nchi zote duniani kuridhia nakulipitisha.
 
Pia ametoa wito kwa nchi zilizo pitisha Azimio hilo kwenda mbali zaidi kwa kuweka será za kitaifa na sheria zinazolinda shule, wanafunzi na kuwachukulia hatua wakataohusika na vitendo viovu.
 
Akihitimisha hotuba yake Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amelaani vitendo vya kuvamia shule na kuteka wanafunzi na kuwalazimisha kuwa wapiganaji au wanawake na wasichana kukataliwa haki yao ya kupata elimu.
 Amewahimiza wahisani kusaidia mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNESCO na  lile la kuhudumia watoto UNICEF ili nao waendelee na juhudi za kulinda elimu, wanafunzi na shule zilizoko katika sehemu hatari zaidi ulimwenguni kwani amesema kwa kuwa tukilinda elimu tunalinda kizazi kijacho.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter