Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban waunda serikali isiyo na wanawake, UN Women yasikitishwa

Zaidi ya familia 400 kutoka majimbo ya Kunduz, Sar -e Pol na Takhar wamepatiiwa makazi katika shule ya sekondari kusini mwa Kabul
© UNICEF Afghanistan
Zaidi ya familia 400 kutoka majimbo ya Kunduz, Sar -e Pol na Takhar wamepatiiwa makazi katika shule ya sekondari kusini mwa Kabul

Taliban waunda serikali isiyo na wanawake, UN Women yasikitishwa

Wanawake

Baada ya Jumanne, Taliban kutangaza kuunda serikali isiyo na wanawake, Naibu Mwakilishi wa shirika la wanawake la Umoja wa Mataifa, UN Women nchini Afghanistan amesema "kukosekana kwa uwazi wa msimamo wa Taliban kuhusu haki za wanawake kumezua hofu ya ajabu" ambayo ni "inayoonekana kote nchini Afghanistan. 

Alison Davidian akizungumza  na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwa njia ya video akiwa mjini Kabul, Afghanistan siku moja baada ya Taliban kutangaza kuunda serikali bila ushiriki wa wanawake amesema UN Women wamekatishwa tamaa na uamuzi wa Taliban na kwamba "kuheshimu haki za wanawake ni kipimo kwa mamlaka yoyote ya serikali, na ambayo mamlaka yoyote ya uongozi inapaswa kuhukumiwa kwayo. Kwa tangazo Taliban imekosa nafasi muhimu kuonesha ulimwengu kwamba kweli wana nia ya kujenga jamii inayojumuisha na yenye mafanikio. " 

Aidha Bi Davidian ameongeza kusema, “ukosefu wa uwazi wa msimamo wa Taliban kuhusu haki za wanawake umesababisha hofu ya ajabu. Hofu hii inaonekana kote nchini. Kumbukumbu ni wazi juu ya jukumu la Taliban katika miaka ya 1990 ambapo kulikuwa na kizuizi kikali juu ya haki za wanawake na wanawake na wasichana wanaogopa. Na hofu hizi zinatokana na ukweli kwamba Taliban bado haijaelezea kikamilifu msimamo wake wa haki za wanawake. " 

Akieleza hali halisi wanayokumbana nayo wanawake wa Afghanistan, Bi Davidian anasema,“kila siku tunapokea ripoti za kurejea nyuma kwa haki za wanawake. Wanawake wamekatazwa kutoka nyumbani bila mahram yaani msimamizi wa kiume. Katika maeneo mengine wameacha kwenda kazini. Vituo vya ulinzi wa wanawake ambavyo vinatoa huduma muhimu kwa wanawake wanaokimbia unyanyasaji vimeshambuliwa na nyumba salama kwa watetezi wa haki za binadamu wanawake wakiwemo waandishi wa habari na wanaharakati zimejaa.” 

Kwa mujibu wa Naibu Mwakilishi huyo wa UN Women nchini Afghanistan, UN Women wamesema watasalia Afghanistan na kufanya kazi kusaidia wanawake wa nchi hiyo.