Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yafanikisha ujenzi wa soko karibu na kambi ya wakimbizi nchini Msumbiji 

Mji wa Palma umekuwa kitovu cha ukosefu wa usalama katika Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji.
© WFP/Grant Lee Neuenburg
Mji wa Palma umekuwa kitovu cha ukosefu wa usalama katika Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji.

WFP yafanikisha ujenzi wa soko karibu na kambi ya wakimbizi nchini Msumbiji 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP kwakushirikiana na wafanyabiashara wadogo, wamefanikiwa kujenga soko karibu na kambi ya wakimbizi wa ndani ya Masquil Alto nchini Msumbiji na kupunguza adha ya wakimbizi kusafiri umbali mrefu kununua bidhaa.

Video ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP, inamuonesha mzee Castigo Jimmo, mwenye umri wa miaka 75 akitembea kuelekea sokoni umbali wa kilometa 4 kwa ajili ya kununua chakula cha familia yake ya watu 10.

Mzee Jimmo anasema, baada ya kununua bidhaa kwa fedha za msaada wanazopewa na WFP anasubiri kupata mtu mwenye baiskeli kwa ajili ya kumsaidia kubeba mizigo yake kurudi nayo kambini, na humlipa ujira wa makopo matatu au 4 ya mchele.

WFP imeamua kutafuta suluhu kwa kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na kisha wafanyabiashara kujenga soko la kuuza bidhaa na wakimbizi wanafurahia taarifa hiyo.

“Itakuwa kitu kizuri sana, niseme kila mtu katika kambi anatamani tuwe na soko hapa, tunafuraha sana kusikia wanajenga soko hapa kwasababu litatusadia sana.”

Sasa soko la kisasa limejengwa, wananchi wanaweza kuona bei ya bidhaa na kununua kwakutumia card. Na wafanyabiashara nao wanafurahia wateja.

“Kuna eneo zuri hapa na nafasi ya kutosha, na watu wanaweza kununua kwa kujinafasi kama unavyoona hapa watu wananunua kwa uhuru, hakuna kujibana, kuna kuachiana nafasi vizuri na hivyo ni vizuri wanajkinga na maambukizi ya COVID-19

Mwakilishi wa WFP anasema lengo lao limetimia

“Juhudi yetu ilikuwa ni kuwa na soko la uhakika, la wanajamii lililotengenezwa na wanajamii wenyewe, na ndio maana tumefanyakazi kwa karibu na wafanyabiashara wa eneo hili ili kuwaonesha matokeo ya mipango ya kutafuta soko la muda mrefu na muda mfupi ambayo inajielekeza kwa jamii kwa kutengenezwa na wanajamii wenyewe.”

Maduka mengine mawili yanatarajiwa kufunguliwa katika eneo hili, ili kutoa nafasi ya kuwawezesha wakimbizi hawa wandani kununua vyakula vyenye kuwapa lishe bora.