Umoja wa Mataifa waendelea kuwasaidia watu wa Haiti kutokana na tetemeko la Agosti 14

7 Septemba 2021

Umoja wa Mataifa na wadau wake wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kutoa misaada huko Les Cayes, Haiti baada ya tetemeko la ardhi lililoipiga kusini magharibi mwa nchi hiyo tarehe 14 mwezi uliopita likiharibu nyumba na miundombinu, kuua na kujeruhi maelfu ya watu.

Video iliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, katika maeneo ya mji wa Les Cayes nchini Haiti inaanza kwa kuonesha picha zilizopigwa kutoka juu kwa ‘drone’ zikiweka wazi kuwa hali bado ni tete katika mji huu kusini magharibi mwa Haiti. Majengo yameporomoka, ni vifusi kila mahali ingawa juhudi za machine nzito za ujenzi kuondoa vifusi zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi.  

Mfumo wa Umoja wa Mataifa umetambua watu 650,000 wanaohitaji msaada wa kibinadamu. Kati ya watu hawa, 500,000 walio hatarini zaidi watapokea msaada wa dharura wa kuokoa maisha. 

Afisa wa Umoja wa Mataifa anapita akizungumza na watu wa hapa huku akifanya tathimini ya uharibifu.  

Katika eneo jingine jirani, maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM wanagawa misaada ambayo si vyakula yakiwemo mablanketi. Wananchi wamekusanyika hapa, wengine wajawazito, wengine wamebeba watoto na wengine ni wazee.  

Mmoja ni Fleurese Derosiers, Mwanamke mzee mwenye umri wa miaka 80 ambaye amefurushwa katika makazi yake kutokana na tetemeko hili la ardhi anasema,  "Tuna shida nyingi. Nyumba zilianguka, ng'ombe wetu walikufa, watu wamejeruhiwa, tunalala nje. Sijafa ni kwa sababu ya neema ya Mungu. Laiti tetemeko la ardhi lingetokea saa 5 asubuhi, ningekufa. Kuta zilianguka pale pale kwenye kitanda changu, ambapo mimi hulala. Ilikuwa muda mfupi sana. " 

OCHA imeruhusu dola milioni 8 kutoka Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF ili kuharakisha usaidizi kwa watu wa Haiti, wakijikita zaidi katika afya, malazi, na msaada wa maji na kujisafi. Msaada wa ziada utahitajika wakati tathmini kamili itakapokamilika. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter