Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban wasema watahakikisha usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu 

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa UN  katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura akijadili  masuala ya kibinadamu na uongozi wa Taliban huko Kabul, Afghanistan.
OCHA
Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa UN katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura akijadili masuala ya kibinadamu na uongozi wa Taliban huko Kabul, Afghanistan.

Taliban wasema watahakikisha usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu 

Msaada wa Kibinadamu

Kufuatia mkutano kati ya mkuu Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA, Bwana Martin Griffiths na maafisa wa Afghanistan, viongozi hao wa Afghanistan wameahidi kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na kuwezesha upatikanaji wa misaada kwa watu walio katika uhitaji. 

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa mjini New York ni kuwa Martin Griffiths jana Jumapili amekutana mjini Kabul na Mullah Baradar, ambaye kwa mujibu wa vyanzo vya habari atakuwa mkuu mpya wa Serikali ya Afghanistan kujadili msururu wa masuala ya kibinadamu. Mkutano huo umehusisha viongozi wengine wa Taliban. 

“Wakati wa mkutano huo, viongozi wa Afghanistan wameahidi kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kibinadamu, kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu walio katika uhitaji, kuhakikisha uhuru wa kusafiri kwa wafanyakazi wa kibinadamu, kwa jinsia zote yaani wanaume na wanawake, na kushirikiana na jamii ya misaada ya  kibinadamu kuhakikisha utoaji wa misaada kwa watu wa Afghanistan.” Imeeleza taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa.  

Aidha Bwana Griffiths pia ameelezea mshikamano wake na watu wa Afghanistan na akasisitiza kujitolea kwa jamii ya kibinadamu "kutoa msaada na ulinzi" bila upendeleo na kwa uhuru kwa "mamilioni ya watu walio katika uhitaji". 

Vile vile taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Griffiths amesisitiza kuhusu hitaji la wanawake kuchukua jukumu la msingi katika usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kuwataka pande zote kuhakikisha haki zao, usalama na ustawi. 

Bwana Griffiths ambaye amezuru Afghanstan kwa ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amepanga pia kukutana na wawakilishi wa mashirika ya kibinadamu ambayo yanaendelea kufanya kazi nchini Afghanistan kutoka Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali.