Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kushika doria Mashariki mwa DRC si lele mama:Koplo Kapindi MONUSCO 

Wanavikosi wa MONUSCO wakipiga doria mkoa wa Ituri nchini DRC.
MONUSCO
Wanavikosi wa MONUSCO wakipiga doria mkoa wa Ituri nchini DRC.

Kushika doria Mashariki mwa DRC si lele mama:Koplo Kapindi MONUSCO 

Amani na Usalama

Machafuko na mashambulizi ya waasi yanayofanywa mara kwa mara Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini wilaya ya Beni, yamekuwa mwiba sio tu kwa raia wa eneo hilo bali pia walindamani wa Umoja wa Mataifa  wanaowajibika kushika doroa kutwa kucha.

Katika kituo cha ukaguzi cha Paida kwenye barabara itokayo Beni kuelekea Kasindi walinda amani kutoka Malawi kikosi cha MALBAT sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kujibu mashambulizi FIB kilicho chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini DRC MONUSCO, wako katika doria ya kila siku. 

Doria wanayolazimika kufanya kila uchao ili kulinda maisha ya raia na mali zao dhidi ya mashambulizi ya waasi. 

Koplo Kumbukani Kapindi ni mmoja wa walindaamani hao wa MALBAT na hapa anafafanua wanachokifanya wakiwa kwenye doria 

“Tunasindikiza magari ya raia kutoka hapa kwenda Kasindi kila siku kama sehemu ya doria. Tunawasindikiza kila siku asunbuhi na kila jioni tunawarejesha hapa.” 

Pamoja na uzoefu wao katika ulinzi wa raia anasema kazi hiyo si lele mama 

“Kuna changamoto kadhaa, mosi ni vigumu kuwabaini waasi kwani wanavaa kama askari kanzu na huwezi kuwatambua, pili ni raia kuna wale wanaoelewa kinachoendelea na wengine hawajui. lakini pamoja na changamoto hizo mambo sio mabaya sana wako salama , kwani tunawasindikiza asubuhi, tunarejesha jioni na usiku tunashika doria.” 

Kwa mujibu wa MONUSCO eneo la Beni ni moja ya maeneo yenye changamoto kubwa za kiusalama nchini DRC na uwepo wa walindaamani kama MALBAT umesaidia kuokoa maisha ya raia wengi.