Mabadiliko ya tabianchi yanasabisha hali mbaya zaidi ya hewa lakini maonyo ya mapema yanaokoa maisha

Kote ulimwenguni mabadiliko ya hali ya hewa yanarekodiwa.
WMO/Daniel Pavlinovic
Kote ulimwenguni mabadiliko ya hali ya hewa yanarekodiwa.

Mabadiliko ya tabianchi yanasabisha hali mbaya zaidi ya hewa lakini maonyo ya mapema yanaokoa maisha

Tabianchi na mazingira

Maafa yanayohusiana na hali ya hewa, tabianchi au majanga ya maji yalitokea katika miaka 50 iliyopita na kuua kwa wastani watu 115 kila siku na kusababisha hasara ya dola milioni 202 kila siku, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa hii leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani, WMO.

Ripoti hii mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO, iliyotolewa leo inaeleza kuwa idadi ya majanga imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 50, ikisababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali mbaya ya hewa lakini kutokana na maonyo bora ya mapema na usimamizi wa majanga, idadi ya vifo ilipungua karibu mara tatu. 

Kwa mujibu wa ramani ya WMO ya Vifo na Upotevu wa Kiuchumi kutokana na Hali ya Hewa, hali mbaya ya tabianchi na Uharibifu wa Maji katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2019, kulikuwa na zaidi ya majanga 11,000 yaliyoripotiwa kuhusishwa na hatari hizi ulimwenguni, na zaidi ya vifo milioni 2 na hasara ya Dola za Kimarekani trilioni 3.64. 

Ripoti hiyo ni tathmini ya vifo na hasara za uchumi kutokana na hali ya hewa, maji na hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi hadi sasa. Ripoti hiyo inatathimini kipindi chote cha miaka 50 na vile vile kwa muongo mmoja mmoja. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuanzia mwaka 1970 hadi 2019, hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatari zitokanazo na maji zilichangia asilimia 50 ya majanga yote, asilimia 45 ya vifo vyote vilivyoripotiwa na asilimia 74 ya hasara zote za kiuchumi zilizoripotiwa. 

“Zaidi ya asilimia 91 ya vifo hivi vilitokea katika nchi zinazoendelea” inaeleza taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani, WMO na ikifafanua zaidi kuwa kati ya majanga 10 ya juu, hatari ambazo zilisababisha upotezaji mkubwa wa binadamu katika kipindi hicho ni ukame, vifo 650,000, Dhoruba, vifo 577 232, mafuriko, vifo 58 700 na joto kali, vifo 55 736. 

Ripoti inasema barani Afrika, ingawa majanga yanayohusiana na mafuriko yalitokea zaidi kwa asilimia 60%, ukame ulisababisha idadi kubwa zaidi ya vifo, ukisababisha asilimia 95 ya maisha yote yaliyopotea katika eneo hilo. 

Vifo vingi vilitokea wakati wa ukame mkali huko Ethiopia mnamo mwaka 1973 na 1983 ikiwa ni jumla ya vifo 400 000, Msumbiji mnamo 1981 ukame ulisababisha vifo 100 000 na Sudan mnamo mwaka 1983 vifo 150, 000.