Kuanza kwa UNGA ni matokeo ya maandalizi ya takribani mwaka mmoja

14 Septemba 2021

Mkutano wa kila mwaka wenye lengo la kuimarisha diplomasia ya kimataifa hufanyika kwa juma moja wakati wa kuanza mwa mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa mataifa lakini maandalizi huchukua miezi kadhaa. Hakuna ambalo halizingatiwi katika tukio ambalo linavuta hisia za mamilioni ya watu duniani kote.

Rais wa nchi hupanda kwenye jukwaa au mimbari ya Baraza kuu la Umoja wa mataifa na kuhutubia mamilioni ya watu. Hiyo ni taswira inayofahamika kwa watu wote ambayo hurudiwa mwishoni mwa mwezi Septemba kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Ambacho hakionekani, ni kazi inayoendelea nyuma ya pazia kuandaa tukio kubwa la kimataifa: Wakuu 193 wa taifa na Serikali, zaidi ya matukio ya pembeni 300, maonesho mengi na wanahabari 5000.

MAANDALIZI NI TAKRIBANI MWAKA MMOJA

Idadi hiyo inaonyesha angalau kwa mukhtasari kazi kubwa iliyoko nyuma yake. Mamia ya wafanyakazi wa Umoja wa mataifa wana jukumu la kuhakikisha wakati mjadala unapoanza tarehe 25 Septemba, kila kitu kiko mahala pake: mipango ya usalama, chakula cha kila utamaduni au bendera sahihi katika kila mkutano.

Maandalizi yanaanza takribani mwaka mmoja hivi kabla. “Tayari watu wamechukua nafasi za mwaka kesho kwa sababu ni chache na zinaenda haraka” anafafanua Fernando Barquín kutoka katika kitengo cha matukio maalumu ambacho kinawajibu wa mipango.

Nchi 193 wanachama zinawasiliana na kitengo cha itifaki cha Umoja wa mataifa kuwafahamisha ni nani atahudhuria kwa niaba ya nchi; kwa kawaida ni mkuu wa nchi au serikali au waziri. Kidogo kidogo jedwali la orodha ya wazungumzaji ambao watashiriki kabla ya Baraza kuu kuanza, huandaliwa. Mtiririko hutegemea na cheo cha muhusika. Kiutamaduni, nchi ya Brazil na Marekani ndizo huanza na zinafuatiwa na wakuu wa nchi, serikali na hatimaye mawaziri. Orodha kila mara inaboreshwa na kwa kawaida kuna mabadiliko mpaka dakika ya mwisho.

Wafanyakazi wa UN wakiandaa bendera tayari kwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la UN.
UN /Ariana Lindquist
Wafanyakazi wa UN wakiandaa bendera tayari kwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la UN.

TIMU TANGULIZI WAKIWEMO WATUMISHI WA MASUALA YA ITIFAKI

Katika wiki za mwanzo, serikali hutuma wale wanaofahamika kama “timu ya utangulizi” hao hufanya mikutano na vitengo mbalimbali vya umoja wa mataifa vinavyohusika. Kisha, wanalizuru jengo la umoja wa mataifa hivyo wanafahamu jinsi ya kuingia katika vyumba tofautitofauti, au kadi maalumu ambazo watazihitaji pamoja na taratibu nyingine.

Ukweli kuwa mkuu wa nchi au waziri anahudhuria si tu inaeleza kuwa atahutubia katika siku za mwanzo wakati ambapo kuna vyombo vingi vya habari vinafuatilia na wawakilishi wengi wapo mkutanoni, lakini pia mapokezi atakayoyapata katika umoja wa mataifa.

Watu wa itifaki huwapokea wawakilishi wote. Wakuu wa nchi na serikali wanapoenda kuhutubia huambatana na maafisa wa umoja wa mataifa ili kuhakikisha kuwa kila mmoja yuko kwenye mimbari wakati sahihi, dakika chache kabla, afisa wa itifaki huambatana nao hadi katika chumba kinachoitwa GA-200. Huko marais husubiri, wakati wanazipitia hotuba zao au wakijipatia kahawa wakisubiri kuitwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa mataifa.

Ni wakati wa heshima ya juu, ambao utakuwa kwenye TV ya Taifa na kimataifa lakini viongozi huudhuria matukio mengi na mikutano.

GUTERRES HUKUTANA NA VIONGOZI WA NCHI NA WAKUU WA SERIKALI GHOROFA YA 39

Mikutano na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kwa kawaida hufanyika ofisini kwake katika ghorofa ya 39 ya makao makuu ya Umoja wa mataifa. Kuna mikutano mingi. Mingi, kiasi hata Katibu Mkuu mwenyewe Antonio Guterres hakuweza kuieleza kwa hakika kwa wanahabari. “Kuna mikutano mia…mia…mia…”, alisema Guterres akiangalia idadi katika karatasi zake mbele ya vicheko vya wanahabari. “Kuna wakuu wa nchi na serikali 132 pamoja na makamu wa rais wanne na mawaziri wa mambo ya nje wapatao 42 hivi” aliwahakikishia baada ya kujumlisha vizuri. “Kalenda bado inapangwa kwa sababu bado ninatakiwa kuongea kwenye matukio 40”

Maafisa wa itifaki huambatana na marais na uhakikisha kuwa bendera za nchi zao ziko katika ukumbi, na kwa upande wa mkuu wa nchi, mfalme au malkia, hupewa mlinzi wa heshima.

Maandalizi ya mlo wa kitaifa ambao huandaliwa na Katibu Mkuu wa UN kwa ajili ya wageni wake.
UN/Kim Haughton
Maandalizi ya mlo wa kitaifa ambao huandaliwa na Katibu Mkuu wa UN kwa ajili ya wageni wake.

MLO WA MCHANA WA KITAIFA

Katibu Mkuu pia hufanya makaribisho jumanne ya tarehe 25 asubuhi saa mbili, na siku hiyo hiyo hufanya dhifa ya chakula cha mchana ambayo huhudhuriwa na wawakilishi wakuu na wakurugenzi kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa. Kila kitu huandaliwa vyema. Vyakula vinapitia ukaguzi mkubwa wa usalama. Orodha ya vyakula huwa pamoja na machaguo kwa ajili ya wasiokula nyama na wale wasiokunywa pombe au kula nguruwe. Eneo ambalo kila mtu hukaa kwenye meza hupangwa kwa uangalifu ili kukwepa mkanganyiko.

Fernando Barquin ameona mipango ya tukio hilo kwa miaka 20 na anathibitisha kuwa hiyo ni siku yenye mambo mengi kuliko wakati mwingine wowote. “Pale ambapo rais wa Marekani anakuwepo, mipango ya usalama inakuwa madhubuti zaidi” anasema. Magari yanayoleta chakula yanaweza kuingia ndani ya Umoja wa mataifa kati ya saa kumi na saa kumi na mbili asubuhi.

 “Ninafika saa kumi na moja (asubuhi) na baada ya shughuli nzima ninatakiwa mara moja kuanza kuupanga upya ukumbi wa chakula kwasababu ni eneo linalohitajika kwa ajili ya matukio mengine.” Hii inaweza kuendelea hadi asubuhi na mapema ya siku nyingine. “Kuna malori sita ambayo ninatakiwa kuyaingiza katika jengo kukusanya samani (viti na meza), lakini siwezi kufanya hivyo mpaka shughuli zote zimeisha na mpaka wana  usalama wanipe ruhusa” anafafanua. “Huwa ni saa tisa au kumi alfajiri.” Barquin anakuja kulala kwenye jengo la Umoja wa mataifa na akiweza kwenda nyumbani ana muda wa kuoga tu haraka na kupata kahawa kabla ya kurejea.

KUFANYA KAZI USIKU

Maandalizi mengi hufanyika kuandaa mkutano mkuu, kwasababu za kiusalama, ni wakati ambapo watu wengine hawaruhusiwi kuingia katika jengo la Umoja wa Mataifa: Usiku na siku za mwisho wa juma.

Wiki chache kabla, muonekano wa maeneo ya Umoja wa Mataifa huanza kubadilika. Katika eneo la kuingia ghorofa ya kwanza ambako kwa kawaida huwakaribisha watalii wengi pamoja na maonesho ya vitu, vyumba vya muda hutengenezwa. “Kuna vyumba 28, vyote vya kufanana, vikiwa na samani za kufanana, ili kusiwe na matatizo ya kiitifaki na yeyote” anasema Barquín. “Kila kimoja kina viti nane, sita vikiwa na kiegemeo kifupi na viwili vikiwa na kiegemeo kirefu kwa ajili ya marais. Meza ya kahawa na meza kwa ajili ya ua na Zulia (Persian rug) ambayo hukodiwa”

Nchi ambazo hufahamika kama P5 yaani wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa (Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China) wana mikutano yao katika eneo lingine ambalo Barquin hana mamlaka ya kulitaja. Amekuwa na Umoja wa mataifa kwa miaka mingi na tayari ameshafahamika miongoni mwa wawakilishi ambao huwasiliana naye kwa ajili ya maandalizi. “Warusi wakati mwingine hunitumia tu ujumbe mfupi wa simu, hawafanyi maombi kwa utaratibu rasmi” anasema.

Nyongeza katika vyumba hivi vya muda, njia ambazo zinaelekea katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viongozi hufungwa, vifaa vya ukaguzi huwekwa, na vyumba vyote ambavyo wageni wakubwa watakuwamo, mapazia ya madirisha hufungwa ili mtu kutoka nje asione wanalolifanya ndani.

MAENEO YA USALAMA.

Suala la usalama ni kazi ya pamoja kati ya Umoja wa mataifa na mamlaka za serikali ya Marekani: Kitengo cha Polisi cha New York na Usalama wa ndani ya nchi.

Maeneo/viunga vya Umoja wa mataifa hufungwa na ni wafanyakazi wa umoja wa mataifa, wageni-walioidhinishwa au watu wanaoishi katika eneo hilo ambao wanaweza kuingia. Magari kuweza kuingia katikati mwa mji wa Manhattan katika siku hizi huwa vigumu.

Msafara wa rais wa Marekani unapopita, ukiwa na zaidi ya magari 12, magari yote mengine na watembea kwa miguu huzuiliwa. Wakati ambapo rais huingia au kuondoka katika makao makuu ya umoja wa mataifa, hakuna mtu mwingine yeyote anaweza kufanya hivyo na hivyo husubiri kwa uvumilivu na kuangalia magari yenye vioo vyeusi na walinzi wenye bunduki wakining’inia kwenye madirisha.

MASHIRIKA YA HABARI KUTOKA KOTE DUNIANI

Mafundi  mitambo  wa video wakifuatilia mjadala wa ngazi ya  juu wakati wa vikao vya Baraza Kuu la  UN
UN /Manuel Elias
Mafundi mitambo wa video wakifuatilia mjadala wa ngazi ya juu wakati wa vikao vya Baraza Kuu la UN

 

Wanahabari 5000 huudhuria katika makao makuu ya Umoja wa mataifa ili kuripoti matukio. Kuna vyombo vya habari kutoka karibu kila nchi duniani.

Kitengo kinachoshughulika na vyombo vya habari kikifahamika kama MALU, huwajibika kuwafahamisha wanahabari kila linalotokea. “Tulishiriki katika mikutano mingi ya kupanga kabla, ambapo tulijaribu kuvipatia taarifa vyombo vya habari: kama wanaweza kuingia, ikiwa wanaweza kupiga picha na video, kama watakuwa na eneo la kukaa” anasema Tal Mekel, mkurugenzi wa kitengo. “Ni changamoto”, anasema.

Ofisini wa kawaida wapo watu tisa, lakini katika juma hili wanawaongeza wafanyakazi wengine nane kutoka katika vitengo vingine au wastaafu-wanaojitolea na huwa na usaidizi wa vijana wengine wadogo 80 ambao wanafanya mafunzo yao ya vitendo katika Umoja wa mataifa. Hawa wana wajibu wa kuwangoza wanahabari kutoka chumba kimoja kwenda kingine ili waweze kufika kwa muda pamoja na kuwepo kwa vizuizi vya kiusalama.

KUTOKA NEW YORK KWENDA DUNIANI KOTE

Nyongeza ni kuwa matangazo ya televisheni ya kila kinachotokea hutumwa kote duniani kwa kutumia mkonga wa mawasiliano. Satelaiti ni aghali zaidi.

 “Tuna njia tano tu na ni changamoto. Mkutano unaokamilika tunauondoa katika mkonga wa mawasiliano kisha tunaweka mwingine. Wakati mwingine warusha matangazo wananipigia simu na ninalazimika kuwaambia kusubiri mpaka siku moja kabla, ili kuona kama nina njia ambayo ninaweza kuitumia kuonyesha mkutano" anasema Martin Redi ambaye anafanya kazi katika kitengo cha Televisheni.

“Kuna mikutano mingi, takribani 100 kwa siku, inachosha,huwezi kuamini” anasema alipoanza kazi kwenye Umoja wa mataifa mwaka 1993 haikuwa mingi. “Sasa hivi kuna matatizo mengi duniani, nchi zote zinahusika katika nchi zingine, katika kanda zao na idadi ya mikutano inaendelea kukukua zaidi na zaidi”.

Timu ya televisheni ambayo ina wafanyakazi wa kudumu kila mwaka, huongezewa nguvu ya mafundi 15 wanaofanya kazi kwa muda wakati wa kipindi cha mkutano.

Siku moja kabla, Redi hutuma mpango kwa warusha matangazo ili waweze kufahamu ni njia gani watajiunga kupata matangazo. Hata hivyo, mpangilio huo unaweza kuwa tofauti, ni muhimu haraka kuwasiliana haraka ili stesheni za televisheni zipate muda wa kuyapata matangazo. “Wakati mwingine wanaweza kuyapata ndani ya dakika kadhaa kwa sababu kuna mikutano kama ile ya dharura ya baraza la usalama ambayo inaweza kutangazwa dakika 15 kabla,” anasema. Kama wasipounganisha moja kwa moja, matangazo yaliyorekodiwa hutumwa kwao na huyapata ndani ya sekunde kadhaa.

Wafanyakazi wakionekana wakiandaa makabrasha ya kutia saini kwa ajili ya makubaliano kati ya nchi.
UN /Manuel Elias
Wafanyakazi wakionekana wakiandaa makabrasha ya kutia saini kwa ajili ya makubaliano kati ya nchi.

 

KAMERA KARIBU KILA UKUMBI

Ili kurekodi kila kitu kinachotokea, kuna kamera katika kila kumbi za mikutano za Umoja wa Mataifa. “Ni zile tunazoziita ‘kamera za roboti’. Kila kiti katika ukumbi kina kipaza sauti na kitufe kidogo. Wakati mshiriki anapokibonyeza kitufe, kamera inalenga moja kwa moja mahali kipaza sauti kilipo” anafaafanua Redi.

Katika mikutano muhimu kuna muongozaji ambaye huongoza kupata picha kwa upana au kuonesha anachofanya mtu akitajwa.

Ni kawaida kwa mabalozi kuongea na wanahabari kabla au baada ya mikutano. Ndiyo maana mara zote kunakuwa na kamera ikiwa tayari. “Hapo ndipo habari nyingi hutengenezwa” anasema Redi.

Kwenye ghorofa ya 39 pia kuna kamera za kurekodi salamu kati ya Katibu Mkuu na viongozi anaowapokea. Redi yuko pembeni kupokea simu, kupokea taarifa kutoka kwa msemaji wa Katibu Mkuu na kuzifahamisha Televisheni ambazo zinapenda kutumia taarifa hizo. “Kila vyombo vya habari vya nchi fulani vinataka picha ya kiongozi wao akiwa na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa na kila moja ni muhimu na wanataka taarifa sasa” anasema.

Siku zake za kazi wakati huu, kama zilivyo za karibia kila mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa anayefanya kazi katika tukio, zinaongezeka. “Inachosha akili, lakini ni uchovu mzuri” anasema Barquín.

NB:Ilichapishwa mara ya kwanza katika wavuti huu mnamo tarehe 20 Septemba 2019

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter