Skip to main content

Kemikali ya risasi yaondolewa kwenye petroli duniani kote.

Baada ya kampeni ya miaka 20 matumizi ya mafuta ya petroli yenye kemikali ya risasi yamekoma ulimwenguni kote, ikiwemo nchini Chad ( kwenye picha)
UN News/Daniel Dickinson
Baada ya kampeni ya miaka 20 matumizi ya mafuta ya petroli yenye kemikali ya risasi yamekoma ulimwenguni kote, ikiwemo nchini Chad ( kwenye picha)

Kemikali ya risasi yaondolewa kwenye petroli duniani kote.

Tabianchi na mazingira

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma ujumbe wa pongezi kwa mshikamano wa serikali za nchi zinazoendelea, wafanyabiashara wakubwa na wananchi wa kawaida kwa juhudi zao za kutokomeza matumizi ya kemikali ya risasi katika mafuta ya petroli. 

Katika ujumbe wake uliotolewa leo mjini New York nchini Marekani Guterres amesema zoezi hili limechukua miaka 20 likisimamiwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP

“Wakati kampeni ya kuondoa kemikali ya risasi ilipoanza, nchi 86 zilikuwa zinatumia petrol yenye kemikali hiyo, lakini leo hakuna nchi hata moja duniani inayotumia. Kutokomeza huku kutaondosha vifo milioni moja vya watoto waliokuwa wanazaliwa kabla ya wakati kila mwaka, matatizo ya moyo, kiharusi, saratani na kutalinda uwezo wa akili wa watoto (IQ ) ambao ulikuwa unaharibiwa kutokana na kemikali hiyo.” 

Guterres amesema kwa mafanikio haya ni wazi kuwa lolote linawezekana iwapo kutakuwa na ushirikiano wa nchi zote duniani ili kufikia lengo mahususi, akitolea mfano itifaki ya Montreal juu ya vitu vinavyoharibu tabaka la ozoni. 

“Mfano mwingine bora ni Itifaki ya Montreal juu ya vitu vinavyoondoa tabaka la Ozoni. Ni lazima sasa tugeukie dhamira ya kumaliza shida tatu kubwa ambazo ni uharibifu wa hali ya hewa, kupotea kwa bayoanuwai na uchafuzi wa mazingira. Tunahitaji kuhama kutoka kwenye matumizi ya mafuta, hadi nishati mbadala. Tunahitaji dunia iendelee kusafiri bila kuwa na uchafuzi wa hewa.” 

Katibu huyo Mkuu amesisitiza lazima ulimwengu ufanye mabadiliko kwenye nishati, mifumo ya chakula na fedha ili kuunda ulimwengu wenye kulindana na sio kuharibu uoto wa asili. 

“Ili kufanikiwa, tunahitaji ushirikiano wa kimataifa, maelewano, mshikamano, tukiongozwa na utaalamu wa kisayansi. Sote tuchukue msukumo huu wa kumaliza matumizi ya madini ya risasi, sote tuelekeze nguvu zetu zote kulinda uoto wa asili, sote tuelekeze nguvu katika ujenzi safi, ulimwengu unaojali mazingira kwa wote.”