Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la kigaidi Kabul ni msumari wa moto juu ya kidonda kwa Waafghanistan:UN

Mtoto akitembea katika kambi ya muda ya Kabul baada ya familia yake kuyakimbia makazi yao kutokana na mzozo nchini Afghanistan
© UNICEF Afghanistan
Mtoto akitembea katika kambi ya muda ya Kabul baada ya familia yake kuyakimbia makazi yao kutokana na mzozo nchini Afghanistan

Shambulio la kigaidi Kabul ni msumari wa moto juu ya kidonda kwa Waafghanistan:UN

Amani na Usalama

Ofisi ya Kamisnina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema shambulio la kigaidi lililofanywa na kundi la ISIL-Khorasan kwenye uwanja wa Ndege wa Kabul nchini Afghanistan jana ni ililikuwa hatua na uamuazi mbaya wa kundi hilo, nani bayana lilikuwa limepangwa kuua na kulemaza watu wengi iwezekanavyo wakiwemo raia, watoto, wanawake, kina baba, kina mama, pamoja na Taliban na vikosi vya kigeni vinavyolinda uwanja wa ndege.

Ofisi hiyo inasema shambulio lililenga kusababisha mauaji na lilifanikiwa kufanya hivyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesisitiza kuwa “hili ilikuwa shambulio la kutisha kwa raia waliokata tamaa, na ofisi ya haki za binadamu inatumai kuwa wale waliohusika watakamatwa na kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.”


 Hali ya kibinadamu

Kwa upande shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema mashambulizi hayo mawili ya kujitoa muhanga katika uwanja wa Ndege wa Kabul yaliyosababisha vifo vya raia zaidi ya 100 wa Afghanistan na wanajeshi 13 wa Marekani huku likijeruhi wengine wengi limeisukuma nchi hiyo katika zahma zaidi ya kibinadamu.

Maelfu kwa amelfu ya watu wamekuwa wakihamishwa kutoka kwenye uwanja wa Ndege wa Kabul katika wiki mbili zilizopita lakini sasa operesheni hizo za usafiri wa anga zinatarajiwa kupungua katika siku chache zijazo kutokana na shambulio hali ambayo UNHCR inasema ni pigo lingine kwa maelfu ya watu wanaotaka kuondoka Afghanistan kwenda kusaka usalama.

Leo shirika hilo la wakimbizi limezindua mpango wa kikanda maandalizi na hatua ambao ni wa kutegemea endapo hali itakuwa mbaya zaidi kwa wakimbizi 500,000 wa Afghanistan kuwasili katika nchi Jirani ifikapo mwisho wa mwaka.

Kwa sasa shirika hilo linahitaji jumla ya dola milioni 299 ili kuliruhusu shirika hilo na mengine ya Umoja wa Mataifa kujipanga kwa misaada na kupokea wimbi kubwa zaidi la wakimbizi.

Nalo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linasema hali bado ni tete nchini Afghanistan na shambulio hilo la jana linaongeza madhila kwa watu ambao tayari wako taaban. Mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuongezeka nchi nzima na sasa watu milioni 18 wanahitaji msaada wa haraka wakikabiliwa na njaa, ukame, vita na COVID-19