Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS waendelea kufanya doroa za barabarani ili kuwalinda wanaofurushwa na mzozo wa kijamii Sudan Kusini 

Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha
UNMISS(Picha ya Maktaba July 2018)
Mlinzi wa kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini kutoka China akiwa anashika doria mjini Juba.Picha

UNMISS waendelea kufanya doroa za barabarani ili kuwalinda wanaofurushwa na mzozo wa kijamii Sudan Kusini 

Amani na Usalama

Walinda amani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS wanaendelea na doria ya barabarani kutoka Tambura hadi Ezo katika Jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini kutathmini hali ya usalama na kibinadamu kufuatia kuzuka kwa mzozo mkali unaoendelea katika eneo hilo.

Magari ya UNMISS yanaonekana yakilazimika kupita katika vinjia vyembamba katikakati ya misitu. Walinda amani wanajaribu kila njia ikiwa ni pamoja na kuweka magogo katika maeneo ya barabara yaliyobomoka ili magari yasikwame, waweze kuwahakikishia usalama wananchi wa Sudan Kusini. 

Mapigano yamelazimisha zaidi ya watu 17,000 kukimbia vijiji vyao katika eneo la Tambura kutafuta hifadhi katika Kaunti jirani ya Ezo. Mmoja wao ni Azande, kijana mdogo wa umri wa miaka 17 akiwa anabubujikwa na machozi anaeleza madhila aliyopitia, 

“Tulikwenda shambani na wazazi wetu ghafla wanaume watatu walitoka msituni. Waliwakamata wazazi wetu, lakini wadogo zangu wadogo watatu wa kiume na mimi tulifanikiwa kukimbia. Tulienda msituni, ambapo tulikaa mpaka usiku. Kisha tukasikia milio ya risasi. Baada ya hapo, niliingia shambani na kukuta miili ya mama na baba imelala.” 

Maafisa wa Ulinzi wa Watoto wa UNMISS wana wasiwasi kuhusu athari zinazowezekana za mzozo wa kijamii unaoendelea. Moses Bagari ni Afisa katika kitengo hicho katika eneo la Yambio anasema,  

"Kuna wasiwasi mwingi wa ulinzi, hasa kwa watoto ambao ndio wako hatarini sana. Hali miongoni mwa wasichana. Inaweza pia kuongeza unyanyasaji wa kingono majumbani na hata uhalifu. Watoto wengi wanaweza kuingizwa katika makundi yenye silaha kwa sababu tumekuwa tukiona vijana wenye silaha karibu na hatuwajui wengi wao." 

Maafisa wa Ulinzi na Usaidizi wa UNMISS nao wana wasiwasi vile vile wanapoendelea kuwasiliana na wahudumu wa masuala ya kibinadamu katika juhudi za kuleta msaada unaohitajika.Thomas Bazawi kutoka kitengo hicho anasema,  “Zaidi ya watu 17,000 katika Kaunti ya Ezo wanahitaji msaada. Moja ya mahitaji ambayo watu hawa waliohama ni ya chakula, kwa sababu hakuna cha kutosha kwa wote. Wanakaa na jamii inayowakaribisha na shinikizo kubwa limewekwa kwenye rasilimali kidogo zilizopo. Lakini wao wanathamini ukarimu unaotolewa na wenyeji wao. Hitaji la pili ni dawa na huduma ya afya. Idadi ya vituo vya afya na uwezo wao hauwezi kuchukua jamii ya wenyeji na watu waliokimbia makazi yao. UNMISS itatumia ofisi yake kuwasiliana na washirika wa kibinadamu wanaweza kuingilia kuokoa maisha ya watoto na wanawake walio katika mazingira magumu.” 

Wakati hali tete ikiendelea, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kulinda wafanyakazi wa kibinadamu wanaotoa huduma kwa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo kubwa la Tambura.