Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhisho lazima zipatikane kwa mamilioni waliokimbia makazi yao Sudan na Sudan Kusini:UNHCR

Vikosi vya UNAMID vikiwa katika doria Darfur
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Vikosi vya UNAMID vikiwa katika doria Darfur

Suluhisho lazima zipatikane kwa mamilioni waliokimbia makazi yao Sudan na Sudan Kusini:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kupata suluhisho zinazotegemea amani na maendeleo ni muhimu kwa mustakabali wa watu karibu milioni saba waliolazimika kuhama kwa nguvu makwao kutoka Sudan na Sudan Kusini, amesema kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi kufuatia ziara yake ya siku tatu katika nchi hizo mbili. 

Wakati wa safari hiyo Bwana Grandi alikutana na waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ambapo walijadili jinsi nchi hizo mbili zinavyoweza kufanya kazi pamoja kusaidia watu wao waliokimbia makazi yao. 

"Kurudi nyumbani ni suluhisho moja lakini sio pekee. Ikiwa mtu anachagua kubaki katika makazi yao, basi mpango huo lazima uhakikishe wanaweza kufanya hivyo kwa utu na hisia za kuwa nyumbani".  

Fursa ya kipekee 

Baada ya serikali za Sudan na Sudan Kusini kutia saini mkataba wa amani uliofufuliwa mnamo 2018, karibu wakimbizi 300,000 wa Sudan Kusini walirudi kiurahisi, na zaidi ya milioni moja wengine waliotawanywa ndani ya nchi hiyo pia wakirudi majumbani mwao. 

Mnamo Juni, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Nicholas Haysom, ambaye pia anaongoza Ujumbe wa Umoja huo huko Sudani Kusini, unaojulikana kama UNMISS, ameonya kwamba ukosefu wa usalama unaoenea haswa vurugu za kijamii unaendelea kukwamisha suluhu ya amani ya kudumu na endelevu na karibu miaka mitatu baadaye, mahitaji mengi ya mkataba uliofufuliwa hayajatimizwa. 

Akihitimisha ziara yake, Bwana Grandi amehimiza kuendelea kuungwa mkono kwa mpango huo, ambao unakusudia kupata suluhisho la kudumu kwa wakimbizi, wakimbizi wa ndani (IDPs), waliorejea na jamii zinazowahifadhi kupitia mageuzi, mabadiliko ya kisiasa, usalama, maendeleo na maridhiano ya kitaifa. 

"Mpango huu ni fursa ya kipekee ya kuweka serikali husika na watu waliokimbia makazi yao katikati ya mipango ya siku za usoni na kwa hivyo, itahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha usalama wao endelevu na usalama". 

Mfano mzuri 

UNHCR imeelezea ni watu waliorejea Sudan Kusini wanarudi na kukuta nyumba zao zimeharibiwa, na miundombinu haitoshi au hakuna huduma za kijamii. 

Regina Ochala ni mmoja wa watu hao ambaye amerejea baada ya kukimbia nyumba yake kaskazini magharibi mwa Wau Sudan Kusini kwa zaidi ya miongo miwili, iliyopita mama huyo wa miaka 42 alitumia karibu maisha yake yote ya  utu uzima katika kambi ya wakimbizi nchini Sudan. 

Alihamia Khartoum kabla ya kurudi nyumbani hivi karibuni ambapo alipanga kuomba msaada kwa kaka yake. Lakini alipofika Juba, aligundua kuwa kaka yake alikuwa amekufa na ndipo alipokwama kimaisha. 

Sasa anajitahidi kukabiliana na maisha nyumbani kwani familia yake yote iliuawa katika vita. 

Suluhisho lazima lipatikane 

Kwa mujibu wa UNHCR, wakimbizi wengi kama Bi Ochala wanahitaji msaada kuanza maisha yao upya katika maeneo salama. 

Bwana Grandi amesisitiza kuwa UNHCR itaendelea kufanya kazi na Serikali za Sudan na Sudan Kusini kwani inategemea msaada wa jamii ya wafadhili wa kimataifa ili kusaidia waliohama na wale waliorejea kuishi kwa usalama, utu na hadhi wanayostahili. 

Amehitimisha kuwa, "Suluhu inapaswa kupatikana kama sehemu ya mchakato wa amani".