Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto bilioni 1 wako hatarini kwa athari za mabadiliko ya tabianchi:UNICEF Ripoti

Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi ya Aden wakiwa wameshika vidumu vya maji. Kambi hiyo hutoa maji mara mbili kwa siku
UN OCHA/GILES CLARKE
Watoto wakimbizi wa ndani katika kambi ya Aden wakiwa wameshika vidumu vya maji. Kambi hiyo hutoa maji mara mbili kwa siku

Watoto bilioni 1 wako hatarini kwa athari za mabadiliko ya tabianchi:UNICEF Ripoti

Tabianchi na mazingira
  • Walio katika hatari zaidi ni kutoka Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Nigeria, Guinea, na Guinea-Bissau
  • Mtoto 1 kati ya 3 ulimwenguni wanaishi katika maeneo ambayo angalau majanga manne ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira yapo au yanaingiliana.
  • Mtoto 1 kati ya 7 duniani kote wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na majanga makubwa matano. 

Vijana na Watoto wanaoishi nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Nigeria, Guinea, na Guinea-Bissau ndio walio katika hatari zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, yakitishia afya zao, elimu, na ulinzi, na kuwaweka kwenye hatari ya magonjwa, kulingana na Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF

Ripoti  hiyo “Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ni mgogoro wa haki za mtoto: Kutambulisha hatari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto” ni uchambuzi wa kwanza wa kina unaotanabaisha hatari ya mabadiliko ya tabianchi kwa mtazamo wa watoto.  
Ripoti inaziweka nchi kutokana na kiwango chake cha hatari ya athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine ya kimazingira kwa watoto kama vile vimbunga na ongezeko la joto, na vile vile kuathiriwa kwao na majanga hayo, kwa misingi ya ufikiaji wao wa huduma muhimu.

 
 Uzunduzi wa ripoti 

Ripoti hiyo iliyozinduliwa kwa kushirikiana na Fridays for future kwenye maadhimisho ya tatu ya harakati za mgomo wa mabadiliko ya tabianchi yanayoongozwa na vijana, imetanabaisha kwamba takriban watoto bilioni 1 karibu nusu ya watoto bilioni 2.2 wanaishi katika moja ya nchi 33 zilizoainishwa kama zenye hatari zaidi ya mabadiliko ya tabianchi .  

“Na watoto hawa wanakabiliwa na kukumbwa na hatari mchanganyiko za mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine ya kimazingira na hivyo kuwaweka katika hatari kubwa kwa sababu ya kutokuwa na huduma muhimu na za kutosha, kama maji na usafi wa mazingira, huduma za afya na elimu.” 

Matokeo ya ripotio hii yanaonyesha idadi ya watoto walioathiriwa wakati huu lakini takwimu zinaweza kuwa mbaya zaidi wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea. 

"Kwa mara ya kwanza, tuna picha kamili ya wapi na jinsi watoto wanavyoweza kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, na picha hiyo ni mbaya sana. Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira unadhoofisha wigo kamili wa haki za watoto, kuanzia upatikanaji wa hewa safi, chakula na maji salama, kupata elimu, makazi, uhuru kutoka kwa unyonyaji, na hata haki yao ya kuishi. Karibu maisha ya kila mtoto yataguswa, "amesema Henrietta Fore, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF.  

Ameongeza kuwa “Kwa miaka mitatu, watoto wamepaza sauti zao kote duniani kudai hatua zichukuliwe. UNICEF inaunga mkono wito wao wa mabadiliko kwa ujumbe ulio bayana kwamba mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ni mgogoro wa haki za mtoto. " 

Mkazi wa Les Cayes, nyumba anayoishi iliharibiwa na tetemeko lililotokea tarehe 14 Agosti 2021 nchini Haiti, akitandika blastiki katika makazi ya muda kwenye uwanja wa mpira walipowekwa waathirika wa kimbunga Grace
©UNICEF/UN0503591/Rouzier
Mkazi wa Les Cayes, nyumba anayoishi iliharibiwa na tetemeko lililotokea tarehe 14 Agosti 2021 nchini Haiti, akitandika blastiki katika makazi ya muda kwenye uwanja wa mpira walipowekwa waathirika wa kimbunga Grace

  Mchanganuo wa takwimu za walivyoathirika 

Kwa mujibu wa mchanganuo wa ripoti hiyo ya UNICEF 
Watoto milioni 240 wanakabiliwa na mafuriko ya pwani; 
• Watoto milioni 330 wanakabiliwa na mafuriko ya yatokanayo na mito; 
• watoto milioni 400 wanakabiliwa sana na vimbunga; 
• watoto milioni 600 wako katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza 
• Watoto milioni 815 wako kwenye hatari kubwa ya uchafuzi wa mazingira; 
• Watoto milioni 820 wanakabiliwa na hatari ya ongezeko la joto; 
• Watoto milioni 920 wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji; 
• watoto bilioni 1 wanakabiliwa na hatari ya kiwango kikubwa sana cha uchafuzi wa hewa  

Kwa mujibu wa UNICEF wakati karibu kila mtoto duniani yuko hatarini angalau kutokana na moja ya hatari hizi za hali ya hewa na mazingira, takwimu zinaonyesha kuwa nchi zilizoathirika zaidi zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kwa wakati mmoja au changamoto zinazoingiliana ambazo zinatishia kudumaza hatua za maendeleo yaliyopigwa maendeleo na kuongeza changamoto kwa watoto. 

Inakadiriwa kwamba watoto milioni 850 au 1 kati ya 3 ulimwenguni wanaishi katika maeneo ambayo angalau majanga manne ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira yapo au yanaingiliana. 
 Watoto wapatao milioni 330 sawa na mtoto 1 kati ya 7 duniani kote wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na majanga makubwa matano. 

 Zahma wasioianzisha 

Bi.Fore amesema "Mabadiliko ya tabianchi hayana usawa. Wakati hakuna mtoto anayehusika na kuongezeka kiwango cha joto ulimwenguni, lakini atalipa gharama kubwa zaidi. Watoto kutoka nchi zisizohusika wataumia zaidi ya wote. Hatahivyo bado kuna wakati wa kuchukua hatua. Kuboresha ufikiaji wa watoto kwa huduma muhimu, kama vile maji na usafi wa mazingira, afya, na elimu, kunaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kuishi katika hatari hizi za mabadiliko ya tabianchi.”  

UNICEF inahimiza serikali na wafanyabiashara wasikilize watoto na kuweka kipaumbele katika hatua zinazowalinda kutokana na athari, huku wakiongeza kasi ya kazi kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafu. " 

“Bila hatua za haraka zinayohitajika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, watoto wataendelea kuteseka zaidi. Ikilinganishwa na watu wazima, watoto wanahitaji chakula na maji zaidi kwa kila kitengo cha uzito wa mwili wao, hawawezi kuishi katika hali mbaya ya hewa, na wako hatarini zaidi kwa kemikali zenye sumu, mabadiliko ya kiwango cha joto na magonjwa, kati ya mambo mengine.